WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda Tume kuchunguza taarifa inayoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti Serengeti pamoja na kutafuta kaburi la faru huyo.

Amesema timu hiyo ya wataalamu tayari imeshafika Sasakwa VIP Grumeti kwa ajili ya kutafuta kaburi na kuchukua vinasaba vya masalia ya Faru John na kisha watakwenda kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kuchukua vinasaba vya watoto wake na kisha kuvilinganisha na pembe hiyo kubaini kama kweli pembe aliyopelekewa ni ya faru huyo ama la.
Majaliwa aliyasema hayo jana wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi mkoani Arusha. Ziara hiyo ililenga kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuona utoaji wa huduma kwa wananchi.
Desemba 9 mwaka huu nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam, Majaliwa alipokea taarifa iliyoelezea utaratibu uliotumika kumhamisha Faru John kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Sasakwa Black Rhino Sanctuary iliyoko kwenye Hifadhi ya Grumeti ambapo aliahidi kuifanyia kazi zaidi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe akisoma taarifa hiyo iliyoandaliwa na Kamati ya Taifa ya Kuwalinda Tembo na Faru, alisema hadi kufikia Desemba 2015 wakati faru John anahamishwa alikuwa na watoto 26 (70.2% ya faru wote waliokuwepo ndani ya kreta).
Alisema baada ya kuhamishiwa Sasakwa, Julai 10, 2016 afya ya faru huyo ilidorora na alikufa Agosti 18, mwaka huu. Hata hivyo, aliuagiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kumletea nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru huyo kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Jana Majaliwa alisema, “Tume niliyounda kwa ajili ya uchunguzi wa faru John imetua VIP Grumeti Serengeti kujiridhisha kama kuna kaburi la faru John na kama lipo wachukue vinasaba na baada ya hapo watakwenda Kreta na kuchukua vinasaba vya watoto wa faru John na kuvipima kwa pamoja. Lengo ni kutaka kubaini kama pembe iliyowasilishwa kwangu Desemba 9 mwaka huu ni ya faru John,” alisema.
Alisema wakati faru John akiwa V I P Grumeti taarifa zilisema ni mgonjwa na daktari alipompima mara ya kwanza akabaini hakuwa na ugonjwa wowote.
“Daktari alimpima tena kwa mara ya pili taarifa zikasema tena si mgonjwa, ghafla wakasema amekufa. Hili haliwezekani”.
Waziri Mkuu alisema ameiagiza timu hiyo kufanya kazi ya uchunguzi wa taarifa hizo kikamilifu kwa sababu Serikali imetumia fedha nyingi kuwaleta faru hao kutoka nchini Afrika Kusini, ni lazima nyara hizo za Serikali zilindwe kwa manufaa ya Taifa.
Katika kikao cha kukabidhi taarifa kilichofanyika Desemba 9 mwaka huu, akikabidhi pembe za faru huyo mbele ya Waziri Mkuu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Robert Mande alimweleza kwamba pembe kubwa ya faru John ilikuwa na uzito wa kilo 3.6 na pembe ndogo ilikuwa na uzito wa kilo 2.3.