MASHTAKA 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam yakiwemo ya ufisadi wa mali za kanisa, yamesababisha Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dk Jacob Chimeledya kumvua uaskofu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Dk Valentine Mokiwa.
Hata hivyo Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezokuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na sio askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.

Uamuzi wa kumvua uskofu ulichukuliwa juzi na Askofu Chimeledya baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauriwa na nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kanisa hilo zilieleza kuwa katika kikao kilichofanyika juzi kanisani Ilala, askofu Chimeledya na ujumbe wake walihudhuria kikao cha halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam akatangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Licha ya uamuzi wa kumvua uaskofu, Dk Chimeledya pia aliagiza waraka unaoagiza askofu huyo kuondolewa madarakani, usambazwe kwenye makanisa yote yaliyoko chini ya dayosisi ya Dar es Salaam na usomwe jana kwenye ibada mbele ya waumini.
“Ni kweli kikao hicho kilifanyika jana, Dk Chimeledya alikuja na katibu mkuu na msajili wa kanisa kwenye kikao, lakini tulishangaa kwamba walikuja na askari polisi kinyume na utaratibu wa kanisa, alisoma maamuzi hayo aliyodai yametolewa na nyumba ya maaskofu,”alisema msemaji wa Dayosisi ya Dar es Salaam Yohana Sanga.
Dk Mokiwa agoma kung’oka
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam Padri Jonathan Senyagwa alisema habari hizo sio za kweli na barua ambazo zimesomwa katika baadhi ya makanisa jijini Dar es Salaam zilisomwa kwa makosa.
“Mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi ni yule aliyemwajiri, na mwajiri wa Dk Mokiwa ni Sinodi ya Dar es Salaam...tutatoa tamko hivi karibuni kuthibitisha kwamba askofu wa jimbo bado hajafukuzwa,” alisema Padri Senyagwa.
Alisema waraka ambao umesambazwa na askofu mkuu wa Tanzania haujapitia kwenye halmashauri ya kudumu ya dayosisi ili kupata baraka zake na wala hauna baraka kutoka kwa sinodi ya dayosisi jambo ambalo linaufanya waraka huo ukose sifa za kutekelezeka.
“Ninachokwambia ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Mokiwa, hatuzitambui barua zilizosomwa katika baadhi ya makanisa,” alisisitiza katibu mkuu huyo wa Dayosisi.
Mgomo huo pia ulithibitishwa na Sanga, ambaye alifafanua kuwa juzi kulifanyika kikao kati ya viongozi wakuu wa kanisa na halmashauri ya kudumu ya dayosisi ya Dar es Salaam na kuelezwa na askofu mkuu wa Tanzania Dk Chimeledya hatua ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa jambo ambalo halmashauri iligoma.
“Tulifanyia kikao chetu pale kanisa la Ilala, viongozi wetu wakuu walikuja na polisi wakatusomea huo waraka na kutangaza maamuzi hayo mbele ya halmashauri, lakini maamuzi hayo yaligomewa na wajumbe wa halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam,” alisema Sanga.
Alisema halmashauri iligoma kubariki uamuzi huo kwa sababu kanisa la Anglikana Tanzania lina kanuni na taratibu zake. Alifafanua kuwa waraka wa kumwondoa madarakani Dk Mokiwa lazima upate baraka za halmashauri ya kudumu ya dayosisi na sinodi ya dayosisi.
“Ule waraka tuliupitia na kubaini kuwa hauna baraza za nyumba ya maakofu, wala hauna baraka za halmashauri ya kudumu na Sinodi ya dayosisi ndio maana tuliwakatalia,” alisema Sanga na kuongeza kuwa maamuzi ya kumvua uaskofu Dk Mokiwa yamefanywa na askofu mkuu wa Tanzania, katibu mkuu na msajili wa kanisa na sio vikao vya kanisa.
“Ninachosisitiza hapa ni kwamba askofu wa dayosisi ya Dar es Salaam bado ni Dk Mokiwa, huo waraka uliotangazwa ni ushawishi wa watu wachache wanaotaka kumchafua kiongozi wetu wa Dayosisi,” alisema.
Aombwa ajiuzulu uaskofu Awali tume hiyo iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi yake, baada ya kubaini makosa mengi yaliyofanywa na askofu huyo ilimshauri ajiuzulu wadhifa wake na awe tayari kufanya huduma nyingine ya kumtumikia Mungu.
“Hatua tunayoichukua ni kwa nia njema kabisa ya kulinusu kanisa letu ambalo limekuwa naheshima kubwa hapa nchini na duniani kote,” unasema waraka uliosaniwa na Dk Chimeledya.
Tume hiyo ilichukua uamuzi huo katika kutatua mgogoro uliopo ndani ya dayosisi ya Dar es Salaam:
“Nia yetu ni njema kabisa na hatuna chuki, uhasama wala upendeleo katika jambo hili, ifahamike kuwa vyombo vyote ndani ya kanisa ikiwemo nyumba ya maaskofu vinalifahamu jambo hili vyema, hivyo tulitarajia tutaungwa mkono ili kuisaidia dayosisi yetu ya Dar es Salaam kwenda mbele.”
Pia waraka huo unaeleza kuwa hiyo sio mara ya kwanza kanisa hilo kufanya maamuzi ya namna hiyo na kutoa mfano kuwa hata enzi za askofu Mokiwa akiwa askofu mkuu wa Tanzania alichukua hatua za kulinusuru kanisa lisipotee katika migogoro mbalimbali ikiwemo mgogoro wa dayosisi ya Tanga ambako alimtaka askofu wa dayosisi hiyo ajiuzulu kwa hiyari na alikubali.
Baada ya kutanguliwa uaskofu wa Mokiwa, Dayosisi ya Dar es Salaam itakuwa chini ya uangalizi wa uongozi wa askofu mkuu mpaka taratibu nyingine za kikanuni zitakapokamilika.
“Nina wasii Wakristo wote kwa nieaba ya Bwana Yesu Kristo tuendelee kuwa watulivu katika kuijenga dayosisi yetu na kanisa la Mungu kwa ujumla.”
Waumini Wanena Sylivester Haule ambaye ni mmoja wa viongozi wa kanisa Anglikana Magomeni alithibitisha jana kwamba waraka huo ulisomwa kanisani kwao.
“Nathibitisha kwamba askofu Mokiwa amevuliwa uaskofu kuanzia leo (jana)sio askofu tena. Waraka wa kumvua uaskofu amekabidhiwa jana (juzi) na makanisa yote yaliyoko chini ya Dayosisi ya Dar es Salaam wamesambaziwa barua hiyo ambao kwetu hapa imesomwa leo,” alisema Haule.
Haule alisema tuhuma za askofu huyo zilianzia kwenye halmashauri ya Dayosisi ya Dar es Salaam, baadaye zikafikishwa nyumba ya maaskofu ambayo iliamua kuunda tume kuchunguza mashitaka dhidi ya askofu Mokiwa.
Alifafanua kuwa tume hiyo yenye wajumbe watano chini ya uenyekiti wa askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Tabora Francis Niruka ambayo ilifanya kazi kwa siku 24 kuanzia Mei mpaka Julai, 2016.
Alisema baada ya tume hiyo kufanya uchunguzi ilibaini ukweli wa tuhuma hizo na kuitisha kikao cha nyumba ya maaskofu Novemba 22, 2016 ambako walihudhuria maaskofu 20 na kukubaliana kwamba askofu mwenzao alikuwa wamevunja katiba ya kanisa hilo na alikuwa amekengeuka kiroho.
“Baada ya tuhuma hizo kubainika kuwa za kweli nyumba ya maaskofu ilimshauri ajiuzulu ndani ya siku saba jambo ambalo aligoma kufanya hivyo, jambo ambalo limemlazimisha avuliwe uaskofu na askofu Mkuu wa Tanzania ambaye ndiye mkuu wa maaskofu wote kwa mujibu wa katiba ya kanisa,” alisema Haule.
Mashitaka 10 ya
Mokiwa Askofu Mokiwa Machi 2015 alifunguliwa mashitaka 10 ambayo ni kuizuia dayosisi ya Dar es Salaam kupeleka michango pasipo maelekezo ya sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, kuhamasisha dayosisi kujitoa katika udhamini wa kanisa Anglikana Tanzania (KAT) kwa lengo la kuifarakanisha dayosisi na jimbo kinyume na katiba ya dayosisi.
Mashitaka mengine ni kufuja mali za kanisa na kuingia mikataba kiholela yenye viashiria vya rushwa katika eneo la kanisa la mtoni Buza na miradi mingine, kushindwa kutatua migogoro inayohusu uwekezaji na maadili baina ya dayosisi na mitaa ya Magomeni ambao kuna mgogoro na Benki ya DCB, kanisa la Kurasini na mengine.
Askofu huyo pia anadaiwa kushindwa kutatua migogoro baina ya mapadiri na waumini na kutunza mali za kanisa katika mtaa wa Watakatifu wote Temeke na kutelekeza nyumba ya askofu iliyopo Oysterbay ambako imegeuzwa kuwa yadi ya kuuza magari.
Pia alilalamikiwa kushitakiwa mahakamani na Marehemu Christopher Mtikila na watu wengine watatu kwa kosa la kuwatishia silaha ya moto na kuwapapasa maungoni mwao bila ridhaa yao kinyume na maadili ya kikanisa.
Askofu Mokiwa pia analalamikiwa kuanzisha taasisi ya MEA Foundation iliyomwezesha kupokea fedha nyingi za wafadhili kwa ajili ya maendeleo ya dayosisi, lakini fedha zimefujwa na hesabu za chombo hazikuwahi kukaguliwa.
Tuhuma zingine ni kurejea kwa mchakato wa mapitio ya katiba mpya na kuvuruga mchakato wa awali wa maandalizi ya katiba mpya ya dayosisi kwa kutumia fedha za dayosisi na kutekelezwa askofu msaidizi dayososi ya Katanga Kalemi Maamuzi ya nyumba ya maaskofu Kwa mujibu wa waraka huo ambao unafafanua hatua zilizopitiwa hadi kuchukua hatua ya kumvua uaskofu, unaeleza kuwa halmashauri ya kanisa la Anglikana Tanzania ilibaini kuwa askofu Mokiwa alivunja sheria za nchi na hivyo kuhatarisha kanisa kupoteza mali zake au kushitakiwa mahakamani kwa kuruhusu mabadiliko ya matumzi ya ardhi katika shamba la kanisa la Mtoni Buza eneo la kanisa la St Mariam Kurasini.
Chombo hicho pia kilisema Dk Mokiwa alikiuka na kuvunja sheria ya miunganiko ya udhamini ya katiba ya kanisa Anglikana Tanzania na katiba ya Dayosisi ya Dar es Salaam kwa kutia saini na kuruhusu padri John Mhina ambaye sio mdhamni kutia saini mikataba mikubwa ya uwekezaji katika maeneo ya kanisa anglikana bila kuweka muhuri wala kushirikisha wadhamini. Halmshauri pia ilibaini askofu Mokiwa ameshindwa kutimiza wajibu wake wa uaskofu wake kwa kutelekeza mali za kanisa na kuziacha ziharibike ikiwemo nyumba ya askofu iliyoko Oystebay, Nyumba ya kanisa ya Silver Oak na shamba la Buza.
Alikutwa na hatia ya kutumia vibaya madaraka yake kwa kushindwa kusimamia mikaaba ya uwekezaji katika shamba la kanisa la mtoni Buza, Magomeni na Kurasini. Pia alikutwa na hatia ya kutumia vibaya vyombo vya mamuzi vya dayosisi ili kuhalalisha na kupitisha maamuzia mbayo yalilenga kulidhoofisha kanisa Angalikana Tanzania kwa maslahi binafsi.
Nyumba ya maaskofu pia ilimkuta na hatia ya ufisadi kwa kuruhusu kufunguliwa akaunti yenye jina la Diocese of Dar es Salaam Evangelism katika benki ya ACB ambayo iliingia fedha nyingi na fedha hizo zimetumika zote katika muda mfupi na haijulikani matumizi yake.
Yeye alikuwa mtia saini wa akaunti hiyo na baadhi ya wasaidizi wake. “Nyumba ya maaskofu iliona kuwa lipo kosa kubwa lililofanywa na baba askofu Mokiwa ya kuvunja sheria za nchi na yeye mwenyewe alikiri shitaka linalohusu mikataba mibovu na matumiz mabyaa ya fedha za kanisa,” inasema barua hiyo.