KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mmoja kati ya watu wawili waliotoroka baada ya wananchi kuwabaini wakifukua kaburi la albino na mmoja kudakwa na Polisi, alirejea kufukua ili kutoa viungo usiku ule ule. Bila kujua wananchi waliweka mtego, huku akifukua kutoa viungo, walimvamia na kumpiga hadi kumuua kabla polisi hawajafika eneo la tukio.

Jana, HabariLEO liliandika kuhusu mkazi wa kijiji cha Chapakazi, kata ya Ilembo Wilaya ya Kipolisi ya Mbalizi mkoani Mbeya, Jonas John(28) kushikiliwa na Polisi mkoani Mbeya baada ya kukutwa akifukua kaburi la mtu mwenye ualbino.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, alisema John alikamatwa Januari 4 mwaka huu saa 7 usiku katika kijiji cha Kijiji cha Mumba kilichopo Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya.
Alikamatwa baada ya watu kutoa taarifa Polisi na hadi wananchi na polisi wanafika eneo hilo, wenzake wawili aliokuwa nao walitoroka huku yeye akikamatwa ndani ya kaburi akiwa ameshaufikia mwili tayari kutoa viungo. Baada ya John kukamatwa, wananchi waliweka mtego.
Bila kujua wenzake John ambao inaonesha hawakwenda umbali mrefu, mmoja alirudi kuendelea kufukua mwili huo ili kutoa viungo katika hilo la Sister Osisara aliyefariki dunia mwaka 2010 na kuzikwa katika makaburi ya familia.
Kamanda Kidavashari alisema muda mfupi baada ya watu kuondoka eneo la tukio mmoja watu hao, Yela Amon (30) mkazi wa kijiji cha Italazya wilayani hapo alirejea ufukua kaburi.
Alisema Amon alirejea bila kujua kuwa wananchi waliweka mtego na ndipo wakati akiendelea na shughuli ya kufukua huku mwenzie aliyekimbia nae akiwa haijulikani alipo, alfajiri ikikaribia, wananchi walimvamia na kuanza kumshambulia kwa mawe na fimbo hadi kumuua.
“Nadhani aliporejea makaburini alikuwa na uhakika kuwa watu wote walikwisha ondoka hivyo akajua atakuwa na wasaa mzuri wa kukamilisha azma yao. Hakujua kama wananchi waliweka mtego wakihisi kuwa waliokimbia wanaweza kurudi,” alisema Kamanda.
Alisema, “Wakati akiendelea na shughuli ya kufukua upya kaburi ndipo wananchi hao waliokuwa na hasira walimvamia na kuanza kumshambulia kwa silaha za jadi ikiwemo mawe na fimbo hadi wakamuua”. Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, Osisara aliyekuwa na ulemavu wa ngozi (albino) alifariki dunia Februari 28 mwaka 2010 na kuzikwa Februari 29 mwaka huo kwenye makaburi hayo ya familia.
Kamanda Kidavashari alisema, Chanzo cha tukio la kufukua kaburi ni imani za kishirikina kwani marehemu na wenzake walikuwa wanataka mifupa ya albino.
Alisema mwili wa marehemu Amon umehifadhiwa katika Hospitali Teule Ifisi iliyopo Mbalizi wakati upelelezi ukiendelea ikiwa ni pamoja na kumsaka mtuhumiwa mmoja ambaye haijajulikana aliko tangu walipokimbia awali.
Hata hivyo alisema bado haijafahamika iwapo vijana hao walitumwa na mtu yeyote au walihitaji viungo vya marehemu kwaajili ya kazi gani.
Wakati huo hupo mwanamke Mkazi wa Mikumi, Hilda Sigara(30) alifariki dunia akiwa anapelekwa Hospitali kwa matibabu jana saa 12 asubuhi baada ya kupigwa na nyundo kichwani na mumewe Rebson Tweve(30-35).
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashar, chanzo cha tukio hilo lililotokea katika kata ya Kyela Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela ni wivu wa kimapenzi kwani inasadikiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na mwanaume mwingine.
Mtuhumiwa alitoroka mara baada ya tukio na juhudi za kumtafuta zinaendelea ambapo eneo la tukio kulikutwa nyundo moja, kisu kimoja na fimbo ya muanzi ambavyo vinasadikiwa kutumika katika tukio hilo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya Kyela ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.
Upelelezi unaendelea. Katika tukio jingine Kamanda Kidavashari alisema mnamo Januari tano saa 12:30 asubuhi huko maeneo ya Majengo, Kata ya Nonde, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kuwa Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Edward Peter(60) Mfanyabiashara na Mkazi wa Majengo amekutwa amefariki dunia chumbani kwake.
Alisema mwili wa marehemu haukukutwa na jeraha lolote na umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu wakati Upelelezi unaendelea.
Katika tukio jingine, Januari 4 mwaka huu saa tisa alasiri katika kijiji cha Kiwanja, Kata ya Mbugani, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Abiud Cosmas(18) Mkazi wa Kiwanja Wilayani Chunya alifariki dunia baada ya kuangukiwa na Kifusi cha Mchanga wakati anajaribu kuchimba madini ya dhahabu.
Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.
Wakati huo huo, Mnamo Januari 5 mwaka huu majira ya saa Sita usiku huko Kijiji na Kata ya Mbugani, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Robert Mwaisenye(18) Mkazi wa Mbugani alikutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya manila akiwa ndani ya nyumba yake.
Chanzo cha tukio hili bado hakifahamika, uchunguzi zaidi unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo chake.