KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga amesema pikipiki zinazokamatwa na Polisi na kukaa muda mrefu katika vituo vya Polisi nchini, baadhi huuzwa kwa mnada.
Mpinga alisema pikipiki inapokaa kituoni zaidi ya miezi sita, vituo vya Polisi huandika barua kwa Mahakama kuomba idhini ziuzwe.

“Mmiliki asipojitokeza, zinauzwa kama mali ya kuokotwa kwani hajulikani, mahakama ikitangaza anatafutwa dalali,” alisema.
Alikuwa akifafanua kuhusu pikipiki hizo baada ya kuwepo taarifa kuwa zinauzwa kwa siri na kwa bei ya chini sawa na bure.
Kuhusu usajili wa pikipiki hizo kwa mnunuzi wa pili, Mpinga alisema, atakayenunua pikipiki hizo anapewa nyaraka ambazo ataenda nazo Mamlaka ya Mapato (TRA) kuandikishwa upya.
Hata hivyo, alisema pikipiki nyingi zinazouzwa ni zilizohusika katika ajali na wahusika hawapatikani zaidi ya miezi sita.
Alisema kwa zilizokamatwa kwa makosa ya usalama barabaran, hakuna ambazo zinatelekezwa kwani wamiliki wake huzichukua.
Alisema hata zinazotelekezwa, nyingi wamiliki wake wanashindwa kuzichukua kwa kuwa zimeharibika na hazitengenezeki.
Kuhusu fedha za mauzo ya pikipiki hizo, alisema, hupelekwa Hazina.
Alisema pikipiki hizo haziuzwi kiholela bali kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi la Polisi na kwamba hana takwimu za zilizokwishauzwa wala kiasi cha fedha kwani pikipiki hizo huuzwa vituo vya Polisi.