Diego Costa anataka kuendelea kusalia Chelsea na ni miongoni mwa wachezaji walio tayari kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Engand dhidi ya Hull Jumapili, meneja Antonio Conte amesema.

Costa, 28, aliacha nje ya kikosi kilichoshinda mechi ya wikendi iliyopita dhidi ya Leicester baada yake kuzozana na mmoja wa wakufunzi kuhusu hali yake.
Hayo yalijiri huku kukiwa na uvumi kwamba alikuwa anatafutwa na klabu za Uchina.
Chelsea walisema aliachwa nje kutokana na maumivu ya mgongo, na kwamba alikuwa amefanya mazoezi pekee kwa siku mbili kama sehemu ya juhudi za kumsaidia kupata nafuu.
"Ana furaha kuendelea kutuchezea. Sioni tatizo lolote,2 alisema Conte.
"Nimesikia uvumi mwingi kumhusu Diego, la muhimu sasa ni kwamba alifanya mazoezi nasi wiki hii, hana maumivu mgongoni na anaweza kucheza.
"Yeye ni mchezaji muhimu sana kwetu na sote twajua hilo. Akiwa katika hali nzuri, amekuwa akituchezea."
Costa atapata mkataba mpya? Begovic ataondoka?
Siku chache kabla ya Chelsea kulaza Leicester 3-0 , Costa alikuwa amehusishwa na kuhamia klabu moja ya China kwa £30m kila mwaka.
Mmiliki wa klabu ya Ligi Kuu ya China Tianjin Quanjian alisema alitaka kumnunua Costa lakini sheria mpya kuhusu kuchezesha wachezaji wa nje ya nchi zikamzuia.
BBC imefahamu kwamba Chelsea hawataki kumuuza Costa, ambaye ndiye mfungaji mabao bora wao msimu huu. Mkataba wake ni wa hadi Juni 2019.
Conte hata hivyo hakusema iwapo Costa ataanza mechi hiyo ya Jumapili dhidi ya Hull.
KUhusu mkataba mpya, alisema kwa sasa ni vyema kufikia kuhusu ya sasa.
Hayo yakijiri, Conte amesema klabu hiyo inatathmini ofa kutoka kwa klabu zinazomtaka kipa Asmir Begovic.
Hata hivyo, alisema kipa huyo wa Bosnia, 29, ambaye amehusishwa na kuhamia Bournemouth, ni mchezaji "muhimu sana katika kikosi (cha Chelsea)".