SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amepokea barua ya Dk Abdallah Possi kujiuzulu ubunge. Dk Possi alikuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais.
Possi ameteuliwa kuwa balozi katika kituo atakachopangiwa kazi baadaye.
Katika taarifa yake kwa umma aliyoitoa jana, Spika Ndugai amesema kufuatia barua hiyo ya kujiuzulu ubunge ya Dk Possi, aliyoipokea Januari 20,mwaka huu iliiyozingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 67 (1) (g) na Ibara ya 149, amemwandikia Rais John Magufuli kuwa sasa wabunge wa kuteuliwa na Rais waliopo ni saba na nafasi zilizo wazi ni tatu.

Wiki hii, Rais Magufuli, amemteua Dk Possi kuwa Balozi.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Possi alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu aliyekuwa akishughulikia Ulemavu.
Kutokana na uteuzi huo nafasi ya Naibu Waziri (Ulemavu) itajazwa baadaye. Juzi Dk Dk Possi alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, akieleza kuwa alikuwa amemwandikia barua ya kujiuzulu ubunge Ndugai kutokana na Rais Magufuli kumteua kuwa Balozi.
Akizungumzia juu ya uamuzi wake huo, Dk Possi alisema;
“Hilo swali nimeulizwa na watu wengi kweli na mimi nikasema hebu ngoja niwape challenge, hivi kweli mnadhani nitakuwa mroho kiasi gani, mnajua niko nje halafu mseme sijiuzulu ubunge wakati siwezi ku-practise eeeh, umenielewa?”