Wanajeshi kutoka nchi za magharibi mwa Afrika wameingia kwenye viunga vya mji mkuu Banjul nchini Gambia ikiwa ni sehemu ya Operesheni kuruhusu rais mpya wa nchi hiyo Adama Barrow, kuchukua madaraka.

Wakazi wa mji huo wameonekana wakishangilia wakati msafara wa wanajeshi hao ulipokuwa ukipita.
Aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Yahya Jammeh aliondoka mapema siku ya jumapili ikiaminika kuwa amepewa hifadhi nchini Gine ya Ikweta.
Jammeh ambaye alishindwa uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka jana, ameondoka madarakani baada ya kuwepo shinikizo kutoka jumuia ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS.
Raia wa Gambia wameeleza kile walichodai kuwa ahueni kwa hali ilivyo hivi sasa..na namna walivyofikia tamati kwa amani.
''leo nina furaha, Ndio, kwa sababu Rais Jammeh ameondoka.Sasa kila mtu ametulia, wana furaha leo, nina furaha sana sana'' alieleza raia mmoja