JALADA la kesi ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh milioni 785.6 inayowakabili watu sita akiwemo Mpemba aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli, Yusuf Ali Yusuf, lipo kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Limepelekwa kwa Kamanda Sirro kwa sababu analifanyia kazi kwa ajili ya kulipeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Thomas Simba, Wakili wa Serikali Patrick Mwita amedai upelelezi wa kesi umekamilika, lakini jalada lipo kwa Sirro linafanyiwa kazi na hajui ni uamuzi gani ambao DPP atauchukua, hivyo aliomba kesi iahirishwe.
Wakili wa utetezi Nehemia Nkoko alidai kuwa wamechoshwa na taarifa za kukamilika kwa upelelezi lakini hawaelezwi hatua itakayofata kwenye kesi hiyo.
Hakimu Simba ameutaka upande wa jamhuri kuhakikisha unaharakisha mwenendo wa kesi hiyo ili iweze kwenda katika hatua nyingine.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 11, mwaka huu.
Mbali na Mpemba, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Charles Mahungo, Benedict Kungwa, Jumanne Chima maarufu kama Jizzo , Ahmed Nyagongo na Pius Kulagwa.
Washitakiwa katika kesi hiyo, wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2014 na Oktoba 2016 katika mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa uhalifu kwa makusudi.
Wanadaiwa kujihusisha na mtandao huo kwa kukusanya na kuuza vipande vya meno ya tembo vyenye thamani ya 785.6, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.