Madaktari nchini Kenya wameigomea nyongeza ya mishahara na posho iliyopendekezwa na serikali yao, ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kumaliza mgomo wa madaktari na wahudumu wa afya ambao umedumu kwa takribani mwezi mmoja sasa.

Mgomo huo ambao kwa sasa umelemaza huduma za matibabu katika hospitali na zahanati za umma nchini Kenya, umekuwa ukiishinikiza serikali kuwalipa mishahara itakayokidhi mahitaji ya madaktari na wauguzi hao.

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alikutana na wawakilishi wa chama cha taifa cha madaktari hao mapemna Jumanne wiki hii na kupendekeza nyongeza ya mshahara na marupurupu ya madaktarii kwa angalau $560 (£450).

Hilo lingesababisha madaktari wanaoanza kazi kulipwa takriban $2,000 kila mwezi.

Viongozi wa chama hicho, ambao walikuwa wameahidi kutangaza msimamo leo, walisema pendekezo la serikali linawafaa madaktari lakini kuna baadhi ya mambo ya kuwafaa wananchi ambayo yameachwa nje.

Madaktari wanaitaka serikali kutekeleza makubaliano ya mishahara na marupurupu yaliyotiwa saini mwaka 2013.

Kwenye makubaliano hayo, serikali iliahidi kuongeza idadi ya madaktari, kuongeza pesa za utafiti wa kimatibabu, dawa na vifaa na mitambo katika hospitali za umma.