Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia makaa ya mawe katika Mgodi wa Ngaka, unaomilikiwa na Kampuni ya Tancoal katika kijiji cha Mdunduaro wilayani Mbinga mkoani Ruvuma jana, alipotembelea mgodi huo.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina, aende kufanya uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni halali.
Alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kupokea taarifa na kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.

Waziri Mkuu alisema atamuagiza pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali (CAG) ili apitie mahesabu ya kampuni hiyo tangu mwaka 2011 walipoanza uzalishaji.
“Mbali na CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.
Katika maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kufahamu ni kwa nini kampuni hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70), licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
“Taarifa zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka, lakini rekodi nilizonazo zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza zaidi ya hapo. Mkaguzi wa Hesabu anasema kampuni imepata, hii itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Mlingi Mkucha.
“Desemba 2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza tani 2,000 kwa Kampuni ya Saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Tanzania na ziliuzwa. Mbona ‘financial statement’ zenu zinasema mwaka huo nao mlipata hasara?” “Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alimbana Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC, aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia, wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
Alihoji pia kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Gideon Nassari alikuwa ni mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy Corporation ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC.
“Wewe ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo, lakini hukuona taabu ya kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi wako?” Waziri Mkuu alihoji.
Alimtaka Mkucha apeleke mkataba huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aupitie upya, na hasa kipengele cha kufungua akaunti za NDC kwa kutumia kanuni za Australia na suala la utaratibu wa gawio kwa wanahisa, ambapo kifungu kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa kwa wanahisa.
“Kipengele kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana hesabu za kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” alisema.
Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL, uongeze uzalishaji ili uweze kukidhi mahitaji ya ndani, kwani makampuni mengi yamebaini gharama kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji makaa ya mawe kwa uzalishaji.
“Nimetembelea mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,” alisema.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa serikali haitaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi na kwa maana nyingine, imeongeza wigo wa soko. Lakini, alisema anaona wanakosa teknolojia uchimbaji makaa kwa wingi na kuwataka wafanye haraka kuleta vifaa hivyo vilivyoko bandarini.