Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jan 7, 2017

Tanzania yapata fursa kubwa ya biashara

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
JITIHADA za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan za kuiingiza Tanzania katika mpango mkubwa wa biashara kwenye Bara la Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, umefanikiwa.
Ni baada ya Tanzania kuchaguliwa kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingizwa katika mpango, unaojulikana kama ‘China One Belt, One Road Stratergy’. Nchi nyingine ambazo zimechaguliwa na kuingizwa kwenye mpango huo ni Malaysia, Sri Lanka, Nepal, Bangladesh, Pakistan na Thailand.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, jana, ilisema baada ya Tanzania kuingizwa rasmi katika mpango huo, Makamu wa Rais, Samia ambaye pia mjumbe katika jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa la Kumuwezesha Mwanamke Kiuchumi, akiwakilisha nchi za Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, alikutana na watendaji kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Biashara (TCCIA) na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), kuwaeleza kuhusu muhimu wa Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo.
Makamu wa Rais alisema Tanzania imepata uanachama ndani ya mpango huo, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara wa madini na vito kutoka China, Dk Helen Lau kuhusu manufaa ya mpango huo.
Alisema alimuomba mfanyabiashara huyo, kuisaidia Tanzania kuingia kwenye mpango wa China One Belt, One Road Stratergy, jambo ambalo limefanikiwa.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa mwezi Septemba mwaka 2016, ulifanyika mkutano Guangdong nchini China kujadili maombi ya kujiunga na mpango huo, ambapo Makamu wa Rais alimuomba Dk Helen, kwa niaba ya Tanzania, awasilishe maombi ya kutaka kujiunga.
Kwa bahati nzuri, ombi la Tanzania lilikubaliwa na kupata uanachama katika mpango huo mkubwa wa China One Belt, One Road Stratergy.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Makamu wa Rais alisema kuwa moja ya fursa zinazotolewa na Serikali ya China katika mpango huo, kila nchi mwanachama hupewa vyumba vya ofisi katika jengo linaloitwa 21st Century Maritime Silk Road Expo bila kulipa kodi ya pango kwa miaka mitatu.
Baadhi ya vyumba vya jengo hilo, vitatumiwa na nchi husika kuonesha na kutangaza bidhaa zao. Kufutia Tanzania kuingizwa kwenye mpango huo, Samia aliwaagiza watendaji wa sekta binafsi aliokutana nao Ikulu jijini Dar es Salaam, wajipange na kuweka mikakati ya namna ya kunufaika na mpango huo haraka iwezekanavyo.
Alibainisha kuwa mpango huo wa China One Belt, One Road Stratergy, ulibuniwa na serikali ya China kwa dhamira ya kuzikutanisha jumuiya za wafanyabiashara za Mashariki mwa Bara Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika ili wabadilishane mawazo, kuonesha njia na kupeana ushauri wa jinsi ya kukuza biashara kati ya nchi wanachama wa mpango huo ili kuiwezesha sekta ya biashara, kuchangia vyema kwenye uchumi wa mataifa yao.
Makamu wa Rais alisema baada ya Tanzania kuingia kwenye mpango huo, itanufaika na fedha za mfuko kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu, ambazo zinatolewa kwa nchi zilizojiunga na mpango huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF, Godfrey Simbeye na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar, Taufik Turki walimuahidi Makamu wa Rais kuwa watatumia fursa hiyo ipasavyo ili kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi wanachama wa mpango huo.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP