Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni.
NAIBU wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ameutaka uongozi wa gereza la kilimo la Mollo lililopo katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa utumie fursa za kilimo ili kuwa wazalishaji wakubwa wa chakula na mifugo nchini.

Alisema iwapo watatumia fursa hiyo ya kilimo kwa kuwa ardhi ya mkoa wa Rukwa inafaa kwa kilimo cha chakula kutokana na kuwa na rutuba ya kutosha na hali nzuri ya hewa wanaweza kuwa wazalishaji wakubwa wa chakula na mifugo nchini.
Naibu Waziri Masauni alieleza hayo baada ya kuelezwa kuwa gereza hilo la kilimo lina eneo la ardhi yenye ukubwa wa ekari 11,000 yenye rutuba, lakini imelima eneo dogo huku likiwa limefuga kuku 300 pekee, idadi inayotajwa kuwa ndogo.
Masauni alifanya ziara ya siku moja mkoani Rukwa ambako alizungumza na kusikiliza kero zinazozikabili taasisi zilizopo chini ya wizara yake katika mkoa huo.
“Fanyeni tathmini, andaeni utaratibu utakaowafanya muweze kuzitumia fursa za kilimo zilizopo na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha chakula cha kutosha,” aliagiza.
Awali, Mkuu wa Magereza mkoani Rukwa, Beni Huja, alimweleza Naibu Waziri kuwa mavuno ya msimu uliopita yalikuwa hafifu kutokana na kuchelewa kupokea pembejeo za kilimo na kutoridhisha kwa hali ya hewa.