Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein akimuapisha Dk Maua Abeid Daftari kuwa Mshauri wa Rais -Pemba katika hafla iliyofanyika Ikulu mjini Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Viongozi walioapishwa na Dk Shein katika hafla iliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar ni Dk Sira Ubwa Mamboya ambaye anakuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu.
Wengine ni Zainab Omar Mohammed ambaye anakuwa Mshauri wa Rais wa Masuala ya Jamii, Wazee, Wanawake na Watoto, Dk Maua Abeid Daftari anakuwa Mshauri wa Rais- Pemba na Rahma Ali Khamis ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Gavu.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mawaziri wasio na Wizara Maalumu ambao pia ni Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Shadya Mohamed Suleiman, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji.
Pia, alikuwepo Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud, Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib, Washauri wa Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa serikali.
|
0 Comments