Wabunge nchini Somalia wamchagua spika mpya. Hii ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi wa urais.
Jumla ya wabunge 259 walishiriki zoezi hilo licha ya ulinzi mkali katika jumba la mafunzo ya polisi.

kwa mujibu wa shirika la habari la AP Mohammed Osma Jawari alichaguliwa tena kuwa spika.
Kwa mujibu mfumo wa uongozi wa ukoo unaoendesha siasa za Somalia ,Kuchaguliwa kwa Bw. Jawari ambaye anatokea ukoo wa Digil na Mirifle,kuna maanisha Sharif Hassan Sheikh Adan, ambaye ni rais wa jimbo la Kusini Magharibi atalazimika kujiondoa katika kinyang'anyiro cha urais kwa sababu anatoka ukoo mmoja na spika.
Wagombea wakuu waliosalia wanatoka koo mbili kubwa za Hawiye na Darod.
Uchaguzi wa urais nchini Somalia umeahirishwa mara kadha kufuatia madai ya udanganyifu na matumizi ya vitisho.
Tarehe rasmi ya uchaguzi haijatolewa lakini maafisa wanasema huenda ikawa baadaye mwezi huu wa Januari.
Wabunge ndio wanamchagua rais tofauti na mfumo wa kawaida ambapo wananchi wanashiriki zoezi hilo moja kwa moja.
Taifa hilo liko katika harakati ya kujiimarisha upya baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu miongo kadhaa.
Uhasama kwa misingi ya ukoo na tishio kutoka kwa wanamgambo wa al shabab wanaopinga democrasia ya mataifa ya magharibi umetajwa kuwa kizingiti cha kufikia lengo hilo.
.