Kesi dhidi ya mwanawe kiongozi wa Equatorial Guinea, imeanza nchini Ufaransa muda mfupi uliopita.
Teodorin Obiang, ambaye pia ni makamu wa rais nchini humo, anatuhumiwa kwa kutumia fedha za serikali kufadhili maisha ya anasa katika mji mkuu wa Ufaransa Paris.

Miongoni mwa mali aliyotumia fedha hizo kununua, ni pamoja na majengo ya kifahari yenye kugharimu zaidi ya dola milioni 100, boti la kifahari lenye urefu wa mita 76, na magari mengi ya kifahari kama vile Bugatti, Ferrari na Rolls Royces.
Waendesha mashtaka nchini Marekani tayari wamemlazimisha kupeana mali kadhaa likiwemo jumba lenye thamani ya milioni 30 huko California na katika maskani ya Michael Jackson.
Babake Teodoro Obiang Nguema, amekuwa mamlakani tangu mwaka 1979 na ndiye rais wa Afrika aliyetawala kwa muda mrefu zaidi.