![]() | |
|
RAIS John Magufuli amewapangia vituo vya kazi mabalozi sita kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali akiwamo Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye sasa atakuwa Balozi nchini Brazil.
Aidha, Dk Magufuli amemteua Muhidin Mboweto kuwa Balozi ambaye kituo chake cha kazi kitapangiwa baadaye.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, iliwataja mabalozi hao wengine na vituo vyao vya kazi kwenye mabano ni Balozi Mbelwa Kairuki (China), Balozi George Madafa (Italia), Balozi Fatma Rajab (Qatar), Balozi Profesa Elizabeth Kiondo (Uturuki) na Balozi Dk James Msekela (Geneva – Umoja wa Mataifa).
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, mabalozi hao wataapishwa leo saa 10:30 jioni Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mabalozi hao waliopangiwa vituo vya kazi ni miongoni mwa mabalozi 21 walioteuliwa na Dk Magufuli, Desemba 3 mwaka jana wakiwemo Balozi Samuel Shelukindo, Balozi Joseph Sokoine, Balozi Silima Haji, Balozi Abdallah Kilima, Balozi Baraka Luvanda na Balozi Sylvester Ambokile.
Wengine walikuwa ni Dk Pindi Chana, Rajab Luhwavi, Luteni Jenerali mstaafu Paul Mella, Grace Mgovano, Mohamed Said Bakari, Job Masima, Omar Yusuph Mzee, Matilda Masuka na Sylvester Mabumba.
Wakati huo huo Rais John Magufuli amemteua Dkt. Abdallah Possi kuwa Balozi. Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Dkt. Abdallah Possi itatangazwa baadaye.
Kabla ya uteuzi huo Dkt. Abdallah Possi alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu aliyekuwa akishughulikia Ulemavu.
Kufuatia uteuzi wa Dkt. Abdallah Possi kuwa Balozi, nafasi ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu (Ulemavu) itajazwa baadaye.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amefanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Martin Bille Herman na kukubaliana kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili hasa katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi.
Pia Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini Burundi. “Rais Dk John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo wa Denmark, Martin Bille Herman.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Denmark nchini, Einar Hebogard na Waziri wa Fedha na Mipango (Tanzania) Dk Philip Mpango,” ilieleza taarifa ya Ikulu.
Ilieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Waziri Herman alisema katika mazungumzo hayo wamejadili kuhusu uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Denmark na pia wamekubaliana kuuimarisha zaidi hususani katika masuala ya maendeleo ya kiuchumi.
Rais Mkapa alisema lengo la kukutana na Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni kumpa taarifa juu ya kazi anayoendelea kuifanya ya kuwa mwezeshaji wa mazungumzo ya mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.

0 Comments