WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku saba kuanzia Januari 18, mwaka huu kwa kila mwananchi mwenye silaha katika wilaya ya Kilindi, mkoa wa Tanga na wilaya ya Kiteto mkoani Manyara kuwasilisha silaha yake katika kituo cha polisi ili ihakikiwe upya na kujua umiliki halali wa silaha hizo.

Viongozi wa mkoa wa Tanga na Manyara wametakiwa kusimamia kikamilifu utaratibu huo na kuhakikisha kila mwananchi mwenye silaha katika wilaya hizo katika mikoa yao awe anamiliki kihalali ama la, anaripoti kituo cha polisi ili zikaguliwe upya.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea katika eneo la mgogoro wa mpaka uliodumu kwa muda mrefu kati ya wilaya ya Kilindi na Kiteto, eneo la Lembapuli ambapo alijionea eneo lililofyekwa mpaka upya wa ziada wa kilometa 2.5 kila upande wa wilaya hizo zilizokuwa zikidaiwa na kugombaniwa na wananchi wa pande zote mbili.
Alisema wakuu hao wa mikoa wanatakiwa kufanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kubaini watu wenye silaha na kuhakikisha silaha zote zinapelekwa kituo cha polisi ili zihakikiwe upya na kwamba baada ya hatua hiyo, adhabu kali zitachukuliwa kwa wananchi watakaokaidi agizo hilo.
“Nimepata habari za watu wanamiliki silaha kiholela, nawaagiza wakuu wa mikoa kuanzia leo (Januari 18) natoa wiki moja kila mwenye silaha akaripoti kituo cha polisi ili ikaguliwe upya kwa kushirikiana na kamati zenu za ulinzi na usalama, ”alisema.
Alikemea tabia ya kuwakamata watu hovyo iliyokuwa ikiendelea katika mgogoro huo wa mpaka na kuwataka kuacha mara moja kwa kuwa wananchi hao ni ndugu na ni watanzania wana uhuru wa kufanya shughuli zao sehemu yeyote ili mradi wanafuata sheria, taratibu za maeneo husika na nchi kwa kuwashirikisha viongozi wao.
Sambamba na hilo alisisitiza kuwa mpaka utakaotenganisha wilaya hizo ni mpaka wa kiutawala uliowekwa kwa GN 65 mwaka 1961 na kwamba amefuta mpaka wa kilometa 2.5 uliowekwa kiholela na wilaya za Kilindi na Kiteto ambao ndio chimbuko la mgogoro huo.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alipongeza uamuzi wa waziri mkuu wa kuhakikisha mauaji yanakomeshwa, uporaji wa mali na uharibifu wa nyumba na vitendo vingine ambapo amerejesha hali ya amani na utulivu katika maeneo hayo iliyotoweka kwa miaka mingi.
Kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na alama na Gn nyingine zilizozaliwa kila upande wa wilaya hizo ambazo ndizo zimeleta mgogoro huo baada ya kuzaliwa wilaya ya Kilindi na wilaya ya Kiteto, ambapo awali ilikuwa wilaya moja iliyojulikana kama Masai District ikiwa na wilaya ya Monduli na Simanjiro na baadaye kugawanyisha wilaya hizo.