Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Naibu Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe. Lulu Msham Abdalla wakati alipofika kutembelea Kiwanada cha  Matrekta huko Mbweni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo,(katikati) Waziri wa Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Mhe. Hamad Rashid Mohamed.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,Maliasili,Mifugo na Uvuvi Dkt.Islam Seif Salum  wakati alipofika kutembelea Kiwanada cha Matrekta Mbweni Wilaya ya Magharibi "B" Unguja leo
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kukiendeleza Kiwanda cha Matrekta Mbweni, kwa lengo la kuimarisha sekta ya kilimo pamoja na sekta nyengine za ufundi hapa nchini. 
Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea kiwanda hicho akiwa amefuata na Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi pamoja na watendaji wakuu wa Serikali wakiongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee. 
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa ziara hiyo aliyoifanya akiwa na viongozi wengine wa Baraza la Mapinduzi na Watendaji Wakuu wa Serikali ni ushauri wake wa kuwataka viongozi hao washiriki pamoja ili wapate kujua muelekeo, hatma, nyenzo, wafanyakazi, mambo yanayohitajika pamoja na changamoto zilizopo. 
Akiwa katika ziara yake ya mwanzo ya kikazi tokea kuingia mwaka mpya wa 2017, Dk. Shein alisema kuwa tokea kuanzishwa Kiwanda hicho mnamo mwaka 1966 haikupiga hatua kubwa licha ya juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali kwa mashirikiano ya Serikali ya China na baadae mnamo mwaka 1980 Serikali ya Uholanzi kuziunga mkono ikiwemo kukijengea uwezo wa kiufundi na kiutawala. 
Dk. Shein alisema kazi ya kikiendeleza Kiwanda hicho si ndogo lakini akimnukuu  shujaa wa Ufaransa Napoleon Bonaparte, aliekuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo tokea kufanyika kwa Mapinduzi ya mwaka 1799 alivyosema kuwa “Tulikwenda, Tukaona na Tukashinda”,  basi anaamini mafanikio yatapatikana baada ya ziara hiyo. 
“Tumekuja, tumeona na tutashinda lakini kubwa ni mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali na wafanyakazi wa Kiwanda hichi...tujiandae kubwa lijalo”,alisema Dk. Shein. 
Hivyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa kazi ya kukiendeleza Kiwanda hicho ni ya Serikali peke yake bali inahitaji mashirikiano makubwa kutoka kwa wafanyakazi wa Karakana hiyo kwani hilo linatasidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lilolokusudiwa. 
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali inaweza kufanya wajibu wake katika kuhakikisha Kiwanda hiyo inarudi katika uhalisia wake lakini bila ya mashirikiano ya wafanyakazi wa karakana hiyo lengo halitofikiwa. 
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa yeye na ujembe aliofuatana nao wameona waliyoyaona katika kiwanda hicyo zikiwemo changamoto zilizopo pamoja na zile za wafanyakazi wake na serikali itafanya juhudi ya kuangalia nini kitafanyika na baadae taarifa rasmi itatolewa.

Hata hiyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kutofanya kazi kwa mazoea kwa kuutaka uongozi na wafanyakazi wa Kiwanda hicho kuyaweka vizuri mazingira ya Kiwanda hicho  pamoja na kuviweka vifaa vichakavu katika utaratibu maalum ambapo licha ya changamoto zilizopo lakini Kiwanda hicho kinaweza kuvutia iwapo hatua hizo zitachukuliwa. 
Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed alitoa shukurani za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa ziara yake hiyo ya mara ya pili katika Kiwanda hicho na kueleza jinsi Dk. Shein anavyofanya maamuzi yake kwa mashirikiano kati yake na wasaidizi wake na hakurupuki katika hilo. 
Waziri Mohammed alisema kuwa juhudi za makususdi zimekuwa zikichukuliwa na Wizara yake katika kuhakikisha wakulima wanatatuliwa changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na kuwalimia mashamba yao kwa kutumia matrekta ambapo katika msimu huu tayari asilimi 87 ya mabonde yameshalimwa licha ya uhaba wa vitendea kazi huku akieleza changamoto ya Taasisi kama hiyo kuwa Kitengo. 
Nao wafanyakazi wa Kiwanda hicho katika risala yao iliyosomwa na Mkuu wa Kitengo cha zana za Kilimo, Mohammed Omar Mohammed walisema kuwa wanajivunia ujio wa Rais kwa mara ya pili katika kipindi cha takriban miaka mitatu kwa lengo la kujali kazi ambazo Karakana hiyo inazitekeleza. 
Mkuu huyo wa kitengo alieleza historia ya Karakana hiyo,  hali halisi ya sasa , majukumu yake  ya kuratibu kazi zote zinazohusiana na zana za kilimo huku wakieleza kuwa kiwanda hicho kinatoa huduma za kiufundi kwa zana zote za kilimo za Serikali na za wateja binafsi pamoja na huduma za ufundi ambazo haziusiani na zana za kilimo kwa taasisi za Serikali. 
Wakieleza miongoni mwa majukumu ya Kiwanda hicho ni pamoja na kuendesha mafunzo ya amali ya kiufundi ya nadharia na vitendo kwa vijana ambao wanapenda kupata ujuzi wa kiufundi hasa kwenye fani za umeme na umakanika kwa muda wa miaka miwili. 
Sambamba na hayo, wafanyakazi hao walieleza changamoto mbali mbali zinazowakabili  Kiwandani hapo ambapo mapema Dk. Shein aliitembelea Kiwanda hicho na kupata maelezo kutoka kwa  Wakuu wa Vitengo ambao walieleza changamoto zilizopo ambapo nayeye alitumia fursa hiyo kuuliza masuala kadhaa. 
Mnamo mwaka 1966, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipata msaada wa matrekta 50 kutoka Jamhuri ya Watu wa China pamoja na majembe yake ya kuchimba na kuburuga kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wakulima ambao walikuwa wakilima kwa kutumia jembe la mkono.