Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatatu  Januari mbili, 2017 amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na kukagua baadhi ya miundo mbinu iliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari ya Ihungo  Omumwani iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10,2016.

Mara baada ya ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaaada na kufanya tathmini ya athari ya tetemeko hilo.

”Kila kitu huwa kina mwanzo na mwisho wake ukiwa na harusi huwa kuna kamati ya harusi,ukishamaliza kufunga ndoa kamati ya harusi huwa inavunjwa,na ukiwa kwenye msiba huwa kuna kamati ya msiba na msiba  mkishazika kamati ya mazishi huvunjwa,kamati ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa tano na inawezekana hata kwenye kamati huwa wanalipana posho,sasa nataka hii kamati nayo iishe,yalishapita yamepita”

Aidha Dkt Magufuli amewataka wote walioahidi kuchangia katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa wa Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi hizo ili ziweze kumalizia miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko hilo.

Ameongeza kuwa wale wote wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pia Rais Dkt Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na Serikali kutaka wanafunzi wote wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za serikali.

Dkt Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi katika zao la kahawa ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima.

Balozi wa Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa jitihada za kupambana na rushwa suala ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila malipo jambo linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania kupata elimu bure


Jaffar Haniu

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Kagera.

02 Januari, 2017