MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kuendelea kuwakamata wale wote wanaohusika na vitendo vya mauaji ya wanyamapori ikiwemo tembo.
Gambo amesema hayo katika kijiji cha Slahhamo wilayani Kahama juzi wakati akizungumza na wananchi , baada ya kukagua ujenzi wa bweni la Shule ya Sekondari ya Slahhamo.

Amesema NCAA iendelee kuwakamata wale wote wanaohusika na mauaji ya tembo katika maeneo hayo ambayo ni msitu, wakiwemo wale wanaowawekea sumu wanyama hao ili wafe.
Gambo amesema, haiwezekani wanyama pori wanatoka msituni na kuingia kwenye mashamba ya watu, badala ya wananchi kutoa taarifa kwa wahifadhi, wao wanachukua sheria mkononi na kuwawekea sumu.
Awali, wananchi hao walilalamikia vitendo vya ndugu zao, kukamatwa na kufungwa, kwa mauaji ya tembo hao, huku wengine wakilalamika fidia ndogo, wanazopewa kama kifuta machozi mara baada ya ndugu zao kuuliwa na wanyamapori.
Mmoja kati ya wananchi hao, Ezekiel Kaaya alisema baadhi ya askari wa NCAA wanakamata watu na kuwabambikizia kesi ya mauaji ya tembo lakini baadhi yao hawahusiki na mauaji hayo.
Kaaya alihoji ni kwa nini bweni la shule ya sekondari Slahhamo, haliishi kwa zaidi ya miaka kadhaa sasa wakati lengo la kujenga bweni hilo ni kuwasaidia wasichana wanaotembea umbali mrefu wasome na kutimiza ndoto zao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu, Waziri Morice amesema bweni hilo haijakamilika kwa sababu mbalimbali zilizotokea hapo awali na hivi sasa wanazishughulikia ili wanafunzi waweze kukaa mabwenini na kupata elimu.