SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema lengo lake mwaka huu ni kuhakikisha wanaimarisha sekta ya viwanda ili kupunguza uingizwaji wa bidhaa kutoka nje.
Akihutubia sherehe za Mapinduzi mjini hapa, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema sekta ya viwanda imechangia pato la taifa kwa asilimia 19.8 mwaka 2015 kutoka asilimia 16.8 mwaka 2014, hivyo kuboreshwa kwa sekta hiyo kutaisaidia Zanzibar kuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa kwenda nje ya nchi na kupunguza kuagiza bidhaa kutoka nje.

Alisema viwanda vitatu vinayomilikiwa na watu binafsi, vimeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wake, ambavyo ni kiwanda cha Maziwa kinachomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Salim Said Bahressa, Kiwanda cha Milk Co-operation na kiwanda cha kusaga unga na makonyo.
Dk Shein alisema kiwanda cha karafuu cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kinaendelea na uzalishaji wake pamoja na kiwanda cha matrekta kilichopo Mbweni, nacho kinaendelea na uzalishaji na matengenezo ya matrekta kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo ambayo imepewa kipaumbele.
Pia alisema katika uzalishaji wa mazao ya baharini, Serikali ipo katika mikakati ya kulipatia ufumbuzi soko la mwani, ambapo uzalishaji wake umeshuka kiasi cha kuwavunja moyo wakulima. Alisema Zanzibar ni nchi ya tatu ya uzalishaji wa mwani katika bara la Afrika kwa Kusafirisha mwani jumla ya tani 11,210 zenye thamani ya Sh bilioni 4.7.
Sekta ya biashara Katika hotuba yake, Shein alizungumzia sekta ya biashara, ambapo alisema sekta hiyo imeonesha mafanikio mwaka 2016 na bidhaa zenye thamani ya zaidi Sh bilioni 94 zilisafirishwa kwenda nje, ukilinganisha na mwaka 2015, ambapo bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 45.71 zilishafirishwa nje ya nchi.
Alisema bidhaa zilizoingizwa Zanzibar, zilikuwa na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 167 kwa mwaka 2016 na mwaka 2015 bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 159.94 zilisafirishwa kwenda nje ambayo ni sawa na asilimia saba.
Dk Shein alisema serikali itaendelea kuongeza usafirishaji wa bidhaa pamoja kuimarisha kilimo. Alisema bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 65.13, zilisafirishwa kwenda Bara huku bidhaa zenye thamani ya Sh bilioni 118.66 zilitoka Bara kwenda Zanzibar mwaka 2016.
Uchumi
Akizungumzia suala la kuimarika kwa uchumi wa taifa, Shein alisema pato la taifa limekuwa kwa asilimia 6.6 huku pato la mtu binafsi lilikuwa kwa zaidi ya milioni 1.8.
Pia alisema serikali yake imeweza kuimarika katika ukusanyaji wa mapato, Januari hadi Novemba mwaka 2016 wamekusanya bilioni 441 kupitia vyanzo vya ndani ukulinganisha na bilioni 336 iliyokusanywa mwaka 2015.
“Ni jambo la kujivunia kwa ukusanyaji huo nawapongeza sana Mamlaka ya Mapato kwa juhudi walizoonesha pamoja na Shirika la Maendeleo la Zanzibar ambalo tumepata Sh bilioni 54.53 kutoka kwao,”alisema.
Katika mikakati ya kuimarisha huduma za uchumi na maendeleo, Dk Shein alisema mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume katika eneo la jengo la abiria ambao ulisita, utaanza hivi karibuni baada ya mazungumzo kukamilika na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China.
Alisema mradi huo hadi kukamilika kwake itakiwezesha kiwanja cha ndege cha Abeid Amaan Karume kuwa na hadhi ya kimataifa na kuwa na uwezo wa kupokea watalii wengi zaidi wanaotazamiwa kufikia laki tano ifikapo mwaka 2020.
Afya Kuhusu sekta ya afya, alisema kwa mwaka 2016 wameanzisha vituo vipya vya afya 152, ujenzi wa wodi za mama na watoto.
Alisema kiwango cha malaria kimeshuka kutoka asilimia 0.6 mwaka 2014 hadi 0.4 mwaka 2015/2016. Elimu Dk Shein alisema mwaka 2015 walikuwa na skuli 792 na mwaka 2016 wameongeza idadi na kuwa na skuli 843 sawa na asilimia saba.
Ili kuhakikisha wanapunguza misongamano serikali inadhamiria kujenga skuli tisa za ghorofa Unguja na Pemba. Kwa upande wa vyuo vikuu, Dk Shein alisema wameweza kusajili wanafunzi 7,383 mwaka 2016 kutoka 6,370 mwaka 2015 ambayo ni sawa na asilimia 5.9 na wanafunzi 2,655 wamepatiwa mikopo ambao ni sawa na asilimia 3.7.
Sherehe zilivyofana
Sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefana visiwani hapa huku wananchi na baadhi ya viongozi, wakisisitiza kuendeleza kuadhimishwa na kutukuzwa kwa sherehe hizo ili vizazi vijavyo viweze kujua kwamba nchi hii imekombolewa kwa wazee kupoteza roho zao.
Gwaride la vikosi vya ulinzi likiongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na ufundi na ustawi wa kwata ya kimya kimya na maonesho ya kikosi cha makomando, walionesha uwezo wao wa kupambana na adui, ni baadhi ya mambo yaliyowavutia watu wengi waliohudhuria katika sherehe hizo.
Licha ya kuwepo kwa jua kali lililoambatana na joto, wananchi walijazana katika kiwanja cha michezo cha Amaan. Sherehe za Mapinduzi ziliongozwa na waandamanaji kutoka katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba, waliobeba mabango mbali mbali yaliyobeba ujumbe wenye lengo la kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi hayo.
Aidha wafanyakazi wa wizara na taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano walipita mbele ya mgeni rasmi wakibeba mabango yenye ujumbe mbali mbali wa kulinda na kuyaenzi Mapinduzi hayo.
Simai Mvuma (71)mkazi wa kijiji cha Chwaka alitoa mwito kwa viongozi kuendelea na utaratibu wa kusherehekea sherehe hizo kila mwaka kwa lengo la kuwakumbusha vijana wa sasa tunatoka wapi na hapo nyuma tulikuwa vipi.
Alipinga mawazo ya baadhi ya watu ambao wanataka kwamba sherehe hizo zisherehekewa baada ya kipindi fulani kwa ajili ya kubana matumizi ya fedha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba alisema Mapinduzi ndiyo yaliyomkomboa Mzanzibari kutoka katika utawala wa Sultani wa Oman.
Alisema Wazanzibari wanayo kila sababu ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sababu ndiyo kielelezo cha watu kuwa huru kwani bila ya Mapinduzi hata Muungano usingekuwepo.
Makamba alikuwepo Zanzibar katika sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi, ambapo alishiriki katika uzinduzi wa kituo cha hifadhi ya msitu wa Mazingini Unguja.
Waziri wa zamani wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ambaye alifanya kazi na marais wa awamu tatu, Ramadhan Abdalla Shaaban, aliwataka wananchi wa Zanzibar kamwe wasitoe nafasi kwa wapinga maendeleo kuyabeza mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Hamad Issa ni mkaazi wa Vitongoji Pemba ambaye alihudhuria sherehe hizo, alisema zimefana kweli kweli huku akifurahishwa na hotuba ya rais ambayo imezidi kutoa muelekeo wa kuimarisha kilimo cha karafuu.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wabunge na wawakilishi.
Imeandikwa na Khatib Suleiman, Zanzibar na Sophia Mwambe, Dar es Salaam.