MKUU wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa, amewatoa wasiwasi wakazi wa mkoa wake kuhusu hali ya chakula, kwa kuwahakikishia kuwa kuna ziada ya tani 461,000 za nafaka.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake kwenye majumuisho ya ziara yake katika masoko makuu ya mjini Musoma kujionea hali ya bei na upatikanaji wa chakula kwa wakazi wa mkoa wa Mara wanaokadiriwa kufikia milioni 1.7.

Alisema mkoa huo una ziada ya tani 461,000 za nafaka zilizovunwa Julai katika msimu wa mwaka jana, chakula ambacho kinaufanya ujihakikishie hali ya usalama wa chakula hadi Mei mwaka huu.
“Hata hivyo, msimu wa mvua za vuli haukutuacha bure kwani tumeendelea kujikusanyia tani nyingine zaidi ya 200,000 za nafaka ambazo zinauhakikishia mkoa kubaki salama kwa chakula hadi Agosti,” alisema.
Alikiri kuwepo kwa ongezeko la bei kwa baadhi ya vyakula vinavyotumiwa kwa wingi na wenyeji na kusema kuwa, hali hiyo itarekebishwa vyakula vitakapoongezeka kwenye masoko.
Dk Mlingwa aliwataka wananchi kuendelea kutumia ziada hiyo ya chakula kwa uangalifu ikiwa ni pamoja na kutotengenezea pombe.
Pia, aliwataka kufanya maadalizi ya kilimo kwakuwa msimu wa masika umekaribia.