Lucy Ngowi KATI ya wanawake 350 na 450 hujifungua kila siku katika hospitali za serikali jijini Dar es Salaam na idadi hiyo haiendani na wauguzi waliopo.
Hali hiyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa na wakati mwingine vifo kwa mtoto anayezaliwa ama mzazi. Idadi ya wauguzi katika mkoa wa Dar es Salaam ni zaidi ya 2,181. Idadi hiyo ni pungufu ukilinganisha na mahitaji halisi ya hospitali husika, kwa kuwa husambazwa katika vitengo mbalimbali vya hospitali husika.

Kuna upungufu asilimia 42 ili kufikia mahitaji halisi ya wauguzi kimkoa. Aidha uwiano uliokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kwamba muuguzi moja mwenye stashahada, shahada ya uzamili na uzamivu, anapaswa kuhudumia wagonjwa kati ya nane na 10.
Kwa yule mwenye cheti, anapaswa kuhudumia wagonjwa wanne hadi sita. Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ziada Sellah alitoa takwimu hiyo ya wanawake wanaojifungua kwa siku baada ya kuulizwa na HabariLeo kutokana na malalamiko mengi yanayojitokeza katika Hospitali za Sinza, Mwananyamala, Amana na Temeke kuwa kuna matukio mengi ya wazazi ama watoto kufariki baada ya kukosa msaada.
Sellah alikiri kupokea malalamiko kuhusu wazazi ama watoto kufariki kutokana na huduma mbovu.
Alisema kuwa wanapopata malalamiko ya mtumishi yeyote ambaye hakutekeleza majukumu yake ipasavyo, huchukua hatua za kinidhamu kwa kumuajibisha ipasavyo kwa kutumia kamati ya maadili ya kituo na manispaa husika.
“Wakati mwingine linapotokea tatizo la mama kutopatiwa huduma nzuri na kusababisha mtoto kunywa maji machafu ama kufariki, tunashindwa kuchukua hatua stahiki kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa mhusika. “Mambo kama haya hutokea, mume anapolalamika baada ya kupata maelezo kutoka kwa mke wake, mke anapoitwa kutoa maelezo anasema hakuna tatizo lolote hivyo kunakuwa hakuna ushirikiano katika ushahidi, jambo hilo linaishia kimya kimya. Kukosa ushirikiano ni tatizo,” alisema.
Sellah alisema idadi ya wanawake wanaojifungua katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam,inapanda na kushuka, lakini mara nyingi kwa hospitali ya Temeke huwa ni kati ya 90 na 100, Amana ni 100 na 120, Mwananyamala ni 60 na 80, Sinza Palestina ni 40 na 60, Mbagala Rangi Tatu ni 40 na 60 na ya Mnazi Mmoja ni 20 na 30 kwa siku.
“Pia kuna zahanati ndogo pamoja na vituo vya afya navyo vinazalisha kati ya akina mama wawili hadi 10 kwa siku na tuna jumla ya vituo 591 vya serikali na vile vinavyomilikiwa na watu binafsi, mashirika ya umma na mashirika ya dini,” alisema muuguzi huyo.
Alisema katika Manispaa ya Temeke kuna wauguzi 474, Kinondoni kuna wauguzi 605, Kigamboni 162, Ilala wauguzi 721 na Ubungo 219 .
Sellah alisema pia bado kuna uhaba mkubwa wa watumishi hasa kada ya uuguzi, ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaopokelewa kwa siku, vile vile idadi ya vitanda hailingani na idadi ya wagonjwa wanaolazwa, hali inayosababisha wagonjwa kulala wawili wawili na katika wodi za watoto wachanga hulala mpaka watatu.
Alikiri kuwepo kwa changamoto nyingi ikiwemo ufinyu wa majengo, idadi kubwa ya wagonjwa isiyolingana na fedha iliyotengwa, hali inayosababisha kuwa na upungufu wa dawa na vifaa tiba mara kwa mara na upungufu wa watumishi.
Alishauri kuongezwa kwa majengo, vifaa tiba na dawa pamoja na watumishi wenye taaluma, waongezwe kulingana na mahitaji ya kila kituo na manispaa.
Akizungumzia suala la wagonjwa kwenda na ndoo au mifuko ya plastiki, alisema kuwa huenda na vifaa hivyo kwa ajili ya kuweka nguo za mama zilizochafuka wakati wa kujifungua kwa sababu hospitali hizo hazina utaratibu wa kufua nguo za wagonjwa walizotoka nazo nyumbani. Alisema hata shuka za hospitali hufuliwa na wazabuni mbalimbali.