Katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi
UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) umebainisha kuwa ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliyopita, ni ishara kuwa Watanzania wanaitambua na kuithamini kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya chama hicho tawala.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi, alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi walioshiriki katika chaguzi hizo, wanachama wa CCM na watendaji kwa kufanikisha ushindi huo.
“Matokeo ya ushindi wa asilimia 75 katika uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Dimani, Zanzibar na ushindi wa asilimia 95 katika kata 20 zilizofanya uchaguzi, Januari 22 mwaka huu, yamedhihirisha bayana imani waliyonayo wananchi kwa Rais John Magufuli,” alisisitiza.
Makilagi alisema tangu Magufuli aingie madarakani ameonesha dhamira ya dhati ya kujenga nchi ili iweze kufikia uchumi wa kati, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za jamii kama vile maji, afya, elimu, miundombinu, reli, usafiri wa anga na majini.
Aliwashukuru wananchi wote walioshiriki katika uchaguzi huo mdogo na kuiwezesha CCM kushinda kwa kishindo katika jimbo na kata 19 za nafasi ya udiwani. Katibu huyo alisisitiza kuwa ushindi huo umetoa picha na mwanga kamili juu ya imani waliyonayo wananchi kwa CCM, lakini pia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.
Hata hivyo, aliwatia moyo watendaji, viongozi, wanachama na wakereketwa wa kata ya Duru, wilayani Babati, mkoani Manyara ambako CCM haikushinda kwenye uchaguzi huo, na kuwataka watembee kifua mbele kwa kuwa CCM ndiyo iliyoshika dola na kuteleza si kuanguka.
Pia aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya ulinzi na usalama kwa maandalizi mazuri ya uchaguzi na kuhakikisha unafanyika kwa salama na amani.
Wakati huo huo, Makilagi aliwaomba wanachama wa umoja huo kushiriki maadhimisho wa miaka 40 ya CCM ambayo UWT imepanga kuadhimisha kwa kufanya kazi za kijamii ikiwemo usafi katika vituo vya huduma za afya na kutembelea vituo vya yatima kwenye ngazi zake zote.
Alisema maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Dodoma, hivyo UWT imejipanga kufanya kazi katika wilaya sita za mkoa huo na wajumbe wa baraza kuu, wa halmashauri kuu ya CCM na wa kamati ya utekelezaji watagawanywa watashiriki katika shughuli hiyo ya usafi.