Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi
MKUU wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, Adam Mgoyi, amesema wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka vijiji vya wafugaji vilivyomo wilayani humo vikiwemo vya Twatwatwa, Ngaite na Parakuyo, hivi sasa wanahesabika kuwa ni wahalifu kutokana na wao kuchangia kwa kiasi kikubwa kuendeleza chuki na uhasama baina yao na wakulima.

Mgoyi alisema tabia ya vijana wao kuendeleza vitendo vya kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima, kuwapiga na kuwatolea vitisho huku viongozi wao wa kimila na dini wakifumbia macho kukemea na kukomesha tabia hizo zinazozidi kushamiri ndani ya wilaya hiyo.
Alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi wa vijiji vya Parakuyo na Twatwatwa ambavyo ni vya jamii ya wafugaji wa Kimasai vilivyopo Tarafa ya Kimamba.
Mkutano uliofanyika Desemba 31, mwaka jana katika kijiji cha Parakuyo na uliitishwa na Mkuu wa Mkoa, Dk Stephen Kebwe ambaye alifanya ziara ya siku mbili wilayani humo, Desemba 30 na 31.
Mkuu huyo wa wilaya alisema wilaya ya Kilosa ina wafugaji wa jamii mbalimbali wakiwemo Wamang’ati, Wasukuma, Wagogo, Wamasai na wengineo.
Alisema wafugaji wa jamii hizo nyingine hawana matatizo na wakulima kutokana na wao kutambua umuhimu wa mazao yanayolimwa na hakuna ugomvi unaoripotiwa kutoka kwa jamii hizo, isipokuwa jamii ya Kimasai wamekuwa na matatizo makubwa kwa kufanya vitendo vya uhalifu.
Alisema jamii ya wafugaji wa Kimasai imekuwa ikifanya vitendo vya uhalifu kutokana na tabia yao ya kupenda kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na tatizo hilo ni kubwa ndani ya wilaya hiyo na kwa sasa limejenga chuki ya pande hizo kuzidi kuongezeka.
“Tatizo kubwa ni la mifugo kuachiwa kwenda kula mazao ya wakulima katika mashamba, lakini wazee wa kimila wa jamii ya Kimasai hawachukui hatua ya kuwakemea watoto wao pale wanapokwenda kinyume na sheria,” alisema Mgoyi na kuongeza.
“Lazima tuambizane ukweli sisi wazee, vijana wenu ni wahalifu, wanalisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima, wanawapinga wanapowakuta mashambani na unapoombwa kutoa ushirikiano muwataje vijana wenu wanaohusika na vitendo vya kihalifu , hamtoi ushirikiano na sasa wote mmechafuka,” alisema Mgoyi.
Hivyo alisema ili kuleta amani na utulivu, ni wajibu wa kwa wazee wa kimila na malaigwanani wa jamii ya wafugaji wa kimasai kuchukua hatua za njia ya kujisafisha kutokana na kuchafuka huko na moja ni kukemea na kudhibiti vitendo vya maovu vinavyofanywa na vijana wao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kushindwa kwao kufanya hivyo kutendelea kuifanya serikali ya wilaya kuwakamata waharifu hao na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Ni vyema tuelewe kuwa jamii mbili hizi zinategemeana, mfugaji anamtegemea mkulima kwa chakula na mkulima anamtegemea mfugaji kwa nyama,” alisema na kuongeza.
Lakini lazima kila upande uheshimu mipaka yake, wafugaji waliingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na wakulima wasiende kulima kwenye maeneo yaliyotengwa kwa vijiji vya wafugaji,” alisema Mgoyi.
Pamoja na hayo alisema, mifugo mingi inayoingizwa katika mashamba ya wakulima ni ya wafugaji wakubwa wakiwemo na viongozi wa jamii hiyo na wengineo na kwa kitendo hicho cha kuchungia kwenye mashamba ya wakulima kimeendelea kuleta machafuko ya mara kwa mara.
“Nimeamua niseme ukweli hapa kwenye mkutano huu kwani wafugaji wakubwa wote wa vijiji vya wafugaji wapo hapa, viongozi wa kidini wa jamii hii pia wapo hapa na sisi wa viongozi wa serikali pia tupo, tusikwepe uozo, kwani mifugo mingi ipo kwenye mashamba ya wakulima kila eneo,” alisema Mgoyi.
Hivyo aliwataka viongozi hao wakomeshe tabia hizo kwa kutaja na vijana wao ili kuwaonya wasiende kulisha mifugo katika mashamba ya wakulima.
Kwa upande wake, Kiongozi wa kimila wa Jamii hiyo katika Kata ya Parakuyo, Abdallah Ngoyai, alisema kuwa pamoja na kuhimiza maadili mema kwa vijana wao baadhi yao wametekwa na mnamo ya kisasa hivyo wanashindwa kufuata maadili na utamaduni wa jamii hiyo.
Ngoyai alitumia fursa hiyo kwa niaba ya jamii hiyo kulaani kitendo kilichofanywa na mmoja wa jamii hiyo kumchoma mkulima mkuki mdomoni uliotokea shingoni kuwa kitendo hicho ni cha kinyama na kimefanywa na wafugaji wachache wenye tabia hiyo na kuichafua jamii yao mbele ya umma wa Watanzania na duniani . Hivyo aliitaka Serikali ichukue hatua kali dhidi yao.