Basi lililokuwa limewabeba watoto wa shule limegonga nguzo ya umemena kushika moto kaskazini mwa Italia.
Maafisa wa huduma za dharura wanasema watu 16 wamefariki.
Basi hilo lilikuwa limewabeba wanafunzi kutoka Hungary na liligonga nguzo ya umeme lilipokuwa linatoka kwenye barabara kuu karibu na mji wa Verona Ijumaa usiku.
Maafisa wa huduma za dharura wa Italia wamesema kwenye Twitter kwamba watu 39 wamejeruhiwa.
Basi hilo lilikuwa safarini kuelekea Budapest kutoka Ufaransa, ambapo wanafunzi hao walikuwa wameenda kwa likizo milimani.
Shirika la habari la Italia Ansa limesema wanafunzi kadha, wengi wavulana, walirushwa nje basi hilo lilipogonga nguzo hiyo.
Wengine walikuwa wamekwama ndani ya basi liliposhika moto, Ansa imeripoti.

Ramani ya Italia, Verona

Idadi ya waliofariki haitarajiwi kuongezeka, maafisa wa huduma za dharura wanasema.