ENEO la ukubwa wa ekari 1,500 limetolewa kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo vya wafanyabiashara mkoani humo.
Ekari hizo zimetolewa na kampuni ya Azimio Estate inayojihusisha na ujenzi wa majengo na uendelezaji wa ardhi na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.

Akizungumza wakati alipotembelea eneo hilo Kigamboni, Makonda amewapongeza kwa kukubali kutoa eneo lao na kusema wameonesha nia ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za nchi kuwa ya viwanda.
Amesema watu wenye viwanda vidogo wana changamoto nyingi za maeneo na wengine kulazimika kuweka katika maeneo ya watu na kusababisha kero kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Aliongeza kuwa baada ya kuona changamoto hiyo waliamua kutafuta wadau wenye maeneo ambao wataweza kutoa mchango wao ili waweze kupata eneo ambao watalitenga kwa ajili ya viwanda vidogo.
“Lengo letu maeneo yatakayopatikana tuyatoe bure kwa makubaliano ya muda fulani yaani wewe mfanyabiashara utafanya shughuli zako kwa miaka kadhaa na utakuwa umekua na kuweza kufika katika kiwanda kikubwa,” amesema Makonda.
Amesema maeneo yatakayopatikana yatafunguliwa Aprili na yatatengwa kwa kila wilaya ambapo maofisa biashara watatakiwa kupita na kuangalia sifa za mtu kupatiwa maeneo ili kuwasaidia wafanyabiashara hao. Makonda pia alitoa mwito kwa watu wenye maeneo kujitolea ili kuunga mkono juhudi za serikali kufikia uchumi wa viwanda.
“Changia ukijua mikono yako ni misafi unalipa kodi vizuri unatenda haki lakini ukitoa kesho ukiwa na jambo lako ukatumia msaada wako kama kichaka cha kujifichia hatutakuacha sababu ya msaada wako, bado sheria itafuata mkondo wake,” alisema.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Mohamed Iqbal amesema, baada ya kupata maombi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa waliamua kutoa ili kusaidia juhudi za serikali za kuwa na viwanda.
“Tulipokea ombi na tumeamua kutoa eneo hili ambao naamini litasaidia katika juhudi hizi za ujenzi wa viwanda vidogo vidogo katika mkoa huu, tutaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wanafikia lengo,” amesema Iqbal.