WATENDAJI wa mitaa na maofisa wa afya katika manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam ambao maeneo yao yatakumbwa na mlipuko wa kipindupindu kwa uzembe wao watawajibishwa kwa kushindwa kusimamia usafi.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Aron Kagurumjuli ametakiwa kuwaandikia barua maofisa watendaji hao ili wajue kuwa atakayeshindwa kusimamia usafi atawajibishwa kwa mujibu wa sheria kwa kuwa atakuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika Kata ya Mzimuni iliyopo Magomeni katika ziara yake ya siku 10 kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi.
Hapi pia amemtaka Mtendaji wa kata hiyoya Mzimuni, Shaban Kambi kuhakikisha anasimamia ipasavyo suala la usafi kwani anaonekana kutosimamia vizuri mfumo wa mapato ya uzoaji taka katika kata yake.
“Mtendaji umeonesha mapungufu makubwa ya kutojua mapato ya ukusanyaji taka yanayotolewa na wananchi, lazima mtendaji na ofisa wa afya kusimamia taratibu za sheria zilizopo na si kuwaacha wananchi kutolipa ushuru wa taka," amesema Hapi.
Amesema kipindi cha mvua kinaanza na kwamba uchafu ni moja ya sababu ya mlipuko wa kipindupindu, hivyo kama mlipuko wa ugonjwa huo utatokea katika mtaa wowote wa manispaa hiyo, watendaji na maofisa afya watawajibika kwa kutotekeleza wajibu wao.
Mtendaji huyo Kambi alishindwa kutoa taarifa sahihi za ushuru wanaotozwa wananchi kwa ajili ya uzoaji wa taka na kwamba anawajibika kusimamia utaratibu waliojiwekea wa kila mwananchi kutoa Sh 10,000 kwa ajili ya taka kila mwezi.
“Katika hili hamtabaki salama mtawajibika, nimeshamuagiza Mkurugenzi kutoa dawa katika visima vifupi na virefu na maeneo ambayo ni hatarishi kwa ajili ya kuua vidudu,” alisema. Katika hatua nyingine, Hapi alimtaka Mkurugenzi wa manispaa hiyo Kagurumjuli anayaondoa malori na magari yote yaliyoegeshwa pembezoni mwa barabara za mitaa kinyume na sheria.
"Magari yote yaliyopaki katika mitaa kinyume ya sheria yatolewe yawe mabovu au malori na kuna wengine mitaa yetu wameifanya kuwa showroom za kuuza magari yao, tunataka mitaa yetu iwe safi,” alisema.
Mtendaji wa kata hiyo ya Mzimuni, Kambi alisema kuwa wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha wanakusanya taka na kwamba makadirio ya taka ngumu zinazozalishwa katika kata hiyo kwa mwezi ni sawa na tani 398.1.
Alifafanua kuwa kati ya taka hizo kiasi kinachopelekwa dampo ni tripu 44 sawa na tani 380 kutoka katika mitaa mine.
|
0 Comments