MKAZI wa Kijiji cha Bisarwi, kata ya Manga, tarafa ya Inano, wilayani Tarime, mkoani Mara, Mwita Nyagosaima (31) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tarime akidaiwa kuvamia usiku nyumbani kwa Magesa Alphonce na kupora bunduki na Sh milioni 5.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa akiwa na panga, baada ya kuvamia nyumbani kwa Alphonce alimtishia kumkata mlalamikaji baada ya kumdhibiti asiweze kutumia silaha yake kujihami na kumpora bunduki aina ya shot gun na Sh 5,000,000 na kutokomea gizani.
Akisomewa mashitaka hayo jana, mbele ya hakimu wa mahakama ya hiyo Amon Kahimba mwendesha mashitaka wa Polisi, Alois Nguluo alidai alidai kuwa mtuhumiwa Nyagosaima Aprili 3 mwaka huu usiku katika kijiji cha Bisarwi alivamia nyumbani kwa Magesa Alphonce akiwa na panga kwa nia ya kutenda kosa hilo.
Alidai kabla Magesa hajajipanga kupambana na mtuhumiwa alitishiwa kukatwa panga na mtuhumiwa na kisha kumpora bunduki yake aliyokuwa akimiliki kihalali yenye namba CAR 641 / 34160 ya thamani ya Sh 850,000.
Mshitakiwa Nyagosaima alikana shitaka lake na upande wa mashitaka ulidai upelelezi bado haujakamilika na hakimu kuamuru kesi hiyo kutajwa tena Mei 2, 2017 na mshitakiwa kwenda rumande hadi tarehe hiyo ya kutajwa.
Katika kesi zingine katika mahakama hiyo wavuvi wawili kutoka mtaa wa Iringo Musoma, Adam Masamba (28) na mwenzake, Revocatus Bornface (41) wamefikishwa katika mahakama hiyo kujibu mashitaka ya kupatikana na nyavu haramu zenye matundu madogo zilizopigwa marufuku hapa nchini katika mwalo wa Kibuyi Ziwa Victoria, wilayani Rorya kwa nia ya kuzitumia katika uvuvi haramu.