SERIKALI imetangaza kuwaajiri mara moja madaktari wote wenye sifa, waliokuwa tayari kwenda kufanya kazi kwa mkataba nchini Kenya.
Uamuzi huo wa Serikali ulitangazwa mjini hapa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Alisema Rais John Magufuli ameamuru madaktari hao waajiriwe mara moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tayari Serikali ilishawapata madaktari 258 waliokuwa na sifa za kwenda kufanya kazi Kenya, baada ya mchujo uliohusisha maombi ya kazi 498 tangu kutangazwa kuwepo kwa nafasi 500 za kazi nchini Kenya Machi 18 mwaka huu na maombi hayo kudumu hadi Machi 27, mwaka huu.

Alisema uamuzi huo umekuja kutokana na madaktari hao, kuwekewa pingamizi mahakamani na wenzao wa Kenya kwenda kufanya kazi nchini humo. “Kwa kuwa utekelezaji wa ratiba ya ajira hizi za madaktari ilikubalika na pande zote mbili kuwa iwe imekamilika ifikapo Aprili 6, 2017 na kuwa madaktari hao wawe tayari kusafiri kwenda nchini Kenya kati ya Aprili 6 na 10, 2017 na kwa kuwa hadi tarehe ya taarifa hii (jana) Mahakama nchini Kenya haijaondoa pingamizi lililofunguliwa dhidi ya madaktari, Rais Magufuli ameamua madaktari hao 258 waajiriwe serikalini mara moja,” alisema.
Aliongeza kuwa awali madaktari hao, hawakuajiriwa serikalini kutokana na uhaba wa fedha. Alifafanua kuwa Rais ndiye mwenye nchi na uwezo wa kujua fedha zinapatikana kutoka wapi, hivyo bila shaka atakuwa amepata uhakika wa fedha za kuajiri wataalamu hao wa sekta ya afya.
Hata hivyo, alisisitiza Serikali itakuwa tayari wakati wowote kushughulikia upya ombi la Serikali ya Kenya la kupatiwa madaktari 500, endapo hakutakuwa na vikwazo vya kuwafanya madaktari wa Tanzania washindwe kwenda kufanya kazi nchini humo.
Machi 18, mwaka huu, Ujumbe wa Serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wake wa Afya, Dk Cleopa Mailu uliowasili nchini ulikutana na Rais Magufuli na aliomba kupatiwa madaktari 500 kwa mkataba wa ajira ya miaka miwili na Rais Magufuli alikubali maombi hayo.
Aidha, kutokana na mahitaji hayo ya madaktari nchini Kenya, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Afya, kushughulikia mchakato wa kuwapata madaktari hao, nayo ikatangaza nafasi za ajira kwa kutumia vigezo kadhaa, ikiwa ni pamoja na waombaji kufanyiwa uhakiki wa vyeti vya taaluma na vyeti vya sekondari, wenye umri usiozidi miaka 55, wenye uzoefu wa kazi, aliyesajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika.
Waombaji walitakiwa pia wasiwe watumishi wa umma, hospitali teule za halmashauri na hospitali za mashirika ya hiyari wanaolipwa mishahara na Serikali. Walitakiwa pia kuonesha vyuo walivyosoma na miaka ya kuhitimu, lakini pia waoneshe sehemu walikofanya mafunzo ya vitendo na miaka waliyohitimu mafunzo hayo.
Kauli ya Madaktari Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk Obadia Nyangole amempongeza Rais John Magufuli kwa agizo la kuwapa ajira madaktari 258 waliotakiwa kupewa ajira nchi ya Kenya. Hata hivyo, amesema mpaka kufikia Oktoba mwaka huu, nchi itakuwa na madaktari 2,883 wasiokuwa na ajira.
Alisema hayo alipohojiwa na gazeti hili kuhusu hatua ya serikali kutangaza kuajiri madakati hao. Dk Nyangole alisema uamuzi huo wa Rais Magufuli ni mzuri na wa haraka na kwamba wao, kama madaktari, wanaupongeza. Lakini, alisema hadi sasa kuna madaktari 1,794 ambao wamemaliza mafunzo, lakini hawana ajira.
Alisema pia kuna wanafunzi 1,809 ambao wamehitimu mafunzo ya udaktari ambapo wapo katika mafunzo ya vitendo, wanayotarajia kumaliza Oktoba mwaka huu. Hivyo, alisema hadi Oktoba kutakuwa na madaktari 2,883 wasiokuwa na ajira.
Obadia alimuomba Rais Magufuli kuwatafutia ajira madaktari katika nchi nyingine za nje, kupitia mabalozi waliopo hapa nchini. Alisema kuwa endapo madaktari hao wa Tanzania, watapata ajira katika nchi za nje, madaktari hao watapata ajira na serikali nayo itapata gawio kupitia mishahara ya watu hao.
Aidha, Dk Nyangole alitaja mikoa 13 nchini yenye uhaba mkubwa wa madkatari, ambapo baadhi yake ni Katavi, Kigoma, Rukwa, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Geita na Manyara.
Ugonjwa wa ajabu Serikali imeelezea kusikitishwa na taarifa za gazeti moja la kila siku (siyo HabariLeo), lenye kichwa cha habari ‘Gonjwa la ajabu linavyoua nchini’. Imesisitiza kwamba taarifa ya gazeti hilo, toleo la jana, inawatia hofu wananchi, kwani ugonjwa wa hemophilia uliotajwa, si mgeni nchini na pia hauambukizi.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Ummy aliyekuwa ameambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Mpoki Ulisubisya, akisema taarifa hiyo inatoa hofu na kuwaaminisha wananchi kuwa pengine ni ugonjwa mpya.
Alisema ugonjwa huo wa kutoganda kwa damu, unasababishwa na vinasaba kama ilivyo kwa magonjwa mengine kama selimundu. Alisisitiza kuwa nchi ina wataalamu wa kutosha, hivyo si tishio kama inavyoelezwa.