Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli
RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa, huku kilio kikubwa cha vyama vya wafanyakazi kikiwa kukosekana kwa mikataba ya hali bora kazini.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na waajiriwa milioni 3.7 katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000 pekee, hali inayoashiria kutokuwa na mikataba.

Katibu Mkuu wa Tucta, Yahaya Msigwa alisema hayo jana mjini Moshi ikiwa ni maandalizi ya Mei Mosi itakayofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU). “Tayari tumemwandikia Rais Dk Magufuli kumuomba awe mgeni rasmi, kimsingi sherehe zote kitaifa mgeni rasmi ni yeye...tunazo ajenda za kumpa Rais, lakini moja ya mambo ambayo ni kero ni hili la mikataba ya hali bora kazini, wafanyakazi wengi wanafanya kazi kama vibarua na hawajui haki zao,” alieleza Msigwa.
Alitolea mfano wa watumishi wa mashambani pekee nchini Kenya ni zaidi ya 700,000 na Afrika Kusini ni zaidi ya milioni moja na kwamba ipo haja kwa waajiri Tanzania kutafakari upya suala la maslahi ya wafanyakazi wao na rais anapaswa kulisemea hilo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Tucta alitaka waajiri kuruhusu kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi ili kutoa fursa kwa wafanyakazi kukutana na kujadili maslahi yao lakini pia kufanya kazi kwa tija zaidi.
Katika hatua nyingine, Msigwa alisema Tucta inaunga mkono kampeni ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupambana na wafanyakazi hewa sanjari na mpango wa kupunguza matumizi ya serikali.
“Pamoja na nia njema ya serikali katika kupambana na wafanyakazi hewa, lakini tunaomba haki itendeke na isitokee mfanyakazi ameonewa kwa namna yoyote ile kwani huko ni kuwakatisha tamaa wafanyakazi waadilifu na waaminifu,” alieleza. Maadhimisho ya Mei Mosi yatahusisha pia kujengwa kwa mabanda ya kuoneshwa kwa shughuli mbalimbali za kisekta nchini.