Jaji Mkuu Kiongozi, Ferdinand Wambali
MAJAJI wa Mahakama Kuu kote nchini wametakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili, uaminifu na uchapakazi uliotukuka ili kujenga heshima na imani kwa wananchi.
Hayo yalisemwa na Jaji Mkuu Kiongozi, Ferdinand Wambali wakati akifungua mafunzo ya wiki moja ya majaji zaidi 60 waliokutana jijini Arusha katika mafunzo ya usimamizi wa uendeshaji wa mashauri, uongozi na usimamizi unaolenga mabadiliko ya kisheria na kuboresha sheria katika utendaji haki.

Alisema wananchi wana imani na Mahakama hususani majaji, hivyo ni vema wakafanya kazi zao kwa kufuata maadili, uaminifu na weledi uliotukuka wenye kufuata misingi ya sheria na utoaji wa haki iliyonyooka.
Aliwataka pia kujiamini katika utendaji kazi wa kila siku na mafunzo hayo yawe chachu zaidi ya kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata misingi ya sheria.
Jaji Kiongozi alisema ujuzi katika mafunzo hayo ni muhimu katika kuboresha mabadiliko ya kisheria na kujenga uwezo wa kufanya kazi kwa kujiamini.
Alisema wananchi wanahitaji huduma nzuri na bora kwa mahakama ikiwa ni pamoja na kupata haki ilinyooka, hivyo majaji wanapaswa kuhakikisha haki inafika kwa wananchi ili kujenga imani hiyo waliyojijengea wananchi kwa mahakama.
Alizungumzia pia mlundikano wa kesi za zamani zisizotolewa maamuzi katika mahakama mbalimbali kote nchini na kusema majaji wafawidhi kote nchini wanapaswa kusimamia na kuhakikisha kesi hizo zinamalizika ikiwa ni pamoja na kutolewa maamuzi ya haki.
“Nataka leo mzungumzie kinagaubaga uendeshaji wa mashauri nini kifanyike kuondoa mlundikano wa kesi mahakamani, na nini kifanyike namna na kuboresha utendaji kazi wa kila siku ili wananchi wapate haki yao bila ya kuyumbishwa,” alisema Jaji Kiongozi.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shangali alisema maelekezo yaliyotolewa na Jaji Kiongozi yatatekelezwa kwa ufasaha ili kujenga imani kwa wananchi kwa mhimili huo wa kutoa sheria.