RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi watambue kwamba huu si wakati tena wa kukaa maskani wakapeana ahadi zisizokuwepo na badala yake wafanye kazi na serikali yao itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwapelekea maendeleo popote pale waliopo.
Aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Mgagadu- Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba, iliyojengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo kazi za ujenzi imefanywa kwa kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kupitia Idara ya Ujenzi na Utunzani UUB.
Katika hotuba yake, alisema wakati wa kupiga siasa umekwisha na kilichokuwepo hivi sasa ni kufanya kazi kwa kila mmoja aliyeajiriwa na asiyeajiriwa na wale wanaojishughulisha na kilimo waendelee na shughuli zao hizo kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Alisema uchaguzi haupo tena hadi mwaka 2020 na kuongeza kuwa vyama vya siasa vipo, lakini hakuna chama kitakacholeta serikali nyingine, kwani tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani ambayo imekuwa ikiwaheshimu na kuwapelekea maendeleo wananchi popote pale walipo.
Alisema yeye ndie Rais wa Zanzibar na kila analosema ana uhakika nalo, kwani hana kawaida ya kusema uongo, hivyo aliendelea kuwaasa wananchi kisiwani humo kuendelea na shughuli zao na kutosikiliza `tumbaku’ za mitaani.
“Wananchi wafanye kazi na zingatieni maelezo ninayosema mbali ya kuwa mimi ndiye Rais wenu pia, ni mwenenu na ndugu yenu…mjue kuwa hapa hakuna serikali nyingine itakayokuja kwani serikali halali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na itaendelea kuwepo,” alisema Dk Shein.
|
0 Comments