WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe jana alitarajiwa kukutana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Bodi ya Ligi (TPLB) na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) huku wakitarajiwa kujadili mapendekezo ya mchakato ya umiliki wa klabu za Simba na Yanga.

Aidha Waziri Mwakyembe amekutana na viongozi wa Klabu ya Simba kusikiliza hoja za mapendekezo ya Klabu hiyo kumilikishwa. Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana mjini hapa, Dk Mwakyembe alisema anakutana na viongozi hao kujadili mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshwaji wa klabu za Simba na Yanga.
Alisema anakutana nao kuona klabu hizo zimekwama wapi kutokana na mapendekezo waliyoyatoa. ‘’Kuna mapendekezo ya mabadiliko ya mfumo ya uongozi ya umiliki katika uongozi wa mpira michakato hiyo imefika wizarani na mimi nikatamani sana nipate picha hii ndio sababu ya kuwaita hapa wenzetu wa BMT, TFF, Msajili wa Vyama vya michezo,’’.
Aidha alisema Aprili 15 mwaka huu alikutana na Baraza la Wazee la Simba likiongozwa na Hamisi Kilomoni ambapo walijadili mchakato huo. ‘’Niliitisha kikao kama hicho na kukaa na wadhamini na wanachama wa Simba katika kiwanja chetu cha taifa waliongozwa na Mzee Kilomoni tuliwasikiliza na kuahidi kukutana nao wiki hii,” alisema.
‘’Leo (jana) jioni nitakaa na viongzi wa Simba kupata picha kamili ili kuendelea na huo mchakato kama walivyofanya Yanga, ndani ya muda mfupi sana tufanye mambo mengine sio masuala ya kutukwamisha tunahitaji tufanye vizuri zaidi katika masuala haya ya michezo,’’ alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa aliishukuru Serikali kwa kuwa karibu na Shirikisho huku akidai wamekuwa wakisaidia katika mambo mbalimbali. ‘’Sisi kama shirikisho tunaishukuru Wizara kwa kutupa ushirikiano kwenye mchakato huu wenye lengo la kujenga mpira uliobora,’’ alisema