Polisi mmoja ameuawa kwa kushambuliwa na risasi mjini Paris nchini Ufaransa na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya mtu mmoja mwenye silaha kulifyatulia risasi basi la Polisi lilipokuwa limeegeshwa katika moja ya mitaa ya mji huo, The Champs Elysees.

Mshambuliaji alitoka kwenye Gari na kuanza kufyatua risasi, huku akijaribu kukimbia eneo la tukio lakini baadae aliuawa na Polisi.
Mwendesha mashtaka jijini Paris, Francois Molins amesema mtu mwenye silaha ametambulika.
Amethibitisha kuwa msako wa Polisi ulikuwa ukiendelea kwenye nyumba ya mshukiwa kwenye viunga vya mashariki mwa Paris.
Alisema Polisi walikuwa wakifanya uchunguzi kuona kama mtu huyo alikua na washirika.
Tukio hilo limetokea siku kadhaa tu kabla ya kufanyika kwa duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais.
Ujumbe uliodaiwa kutoka kwa kundi la wanamgambo wa Islamic State umedai kuwa mmoja wa wafuasi wake Abu Youssef raia wa Ubelgiji alitekeleza shambulio hilo.