Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa.
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeitaka Simba kutokuwa na wasiwasi na badala yake wasubiri kwanza uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji juu ya marejeo ya rufaa dhidi yao iliyokatwa na Kagera Sugar.
Awali, Simba ilishinda rufaa dhidi ya Kagera Sugar kumchezesha Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano na hivyo, timu hiyo ya Kagera ikanyang’anywa ushindi wa pointi tatu na magoli matatu.

Hatua hiyo haikuwaridhisha Kagera na kuomba marejeo ya rufaa hiyo, ambapo TFF iliitisha kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji tangu juzi kusikiliza upya rufaa hiyo. Kitendo hicho kimewafanya Simba kupinga uwepo wa kikao cha Kamati nyingine badala ya ile ya awali kilichotolewa maamuzi na Kamati ya saa 72 wakidai kuwa kufanya hivyo, ni kuwaonea na kutoiamini Bodi ya Ligi.
Akizungumza na gazeti hili jana Katibu Mkuu wa TFF Selestine Mwesiga alisema ni muhimu kwa Simba kuwa watulivu na kutokuwa waoga hadi maamuzi yatakapotoka ndipo wazungumze.
“Zote ni kamati za TFF na kila moja ina nguvu zake. Pale ilipoishia Kamati ya saa 72 ndipo ilipoendelea ile ya Hadhi za Wachezaji,”alisema huku akiongeza kuwa kitendo cha Simba kulalamika kuwa inaonewa na wala kesi zao huwa hazisikilizwi sio cha kweli, kwani wamekuwa wakizungumzia kwenye mitandao badala kufuata utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara aliomba Serikali kuingilia na kumchunguza Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwa kudai kuwa hawatendewi haki.
Alisema iwapo hadi Jumatatu ijayo kama hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya kiongozi huyo, wanaomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi.
“Msimamo wa klabu ya Simba tunataka haki itendeke, kama Malinzi na timu yake wamepanga kuidhulumu Simba tunasema hapatoshi, kwa kuwa Yanga walitishia kwa kusema watamwaga ugali basi na sisi tutamwaga mboga,” alisema.
Alisema wameshawahi kulalamikia mambo mengi na hakuna hata moja lililowahi kufanyiwa kazi. Akitolea mfano suala la mkataba wa mchezaji wa Yanga, Hassan Kessy, suala la Amis Tambwe na Donald Ngoma.
Manara alisema marejeo yaliyotumwa na Kagera Sugar yamepingana na barua ya TFF iliyoitisha kikao cha kamati ya hadhi za wachezaji na sheria. “Kokote pale duniani sio tu Tanzania, marejeo ya shauri yanafanywa na chombo kilichofanya uamuzi wa kwanza, haihitaji kujua sana sheria,” alisema na kufafanua kuwa majereo huwa hauletwi ushahidi mpya na badala yake wanatakiwa kutumia ushahidi ule wa mara ya kwanza.
Alienda mbali zaidi akisema kuwa wanazo taarifa wakati wa kile kikao cha mara ya kwanza cha Kamati ya Saa 72 kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa TFF alitoa taarifa kwa mmoja wa maofisa wake akishinikiza matokeo yale ya awali yasitangazwe na kamati hiyo na kwamba ushahidi wanao.
Msemaji huyo alisema wanashangazwa na kikao hicho cha pili ambacho si cha uhalali kilikaa kwa saa wanazojua wao kikiwahoji meneja, katibu mpaka mchezaji aliyepewa kadi jambo ambalo haijawahi kutokea kokote Pia, alisema wanazo taarifa kuwa jambo hilo limepelekwa kitengo cha makosa ya mtandao kilichoko chini ya Jeshi la Polisi na kwamba kwa nini lisiende Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na vyombo vingine?
Alisema kitendo cha kudhaniwa kuwa wamefoji taarifa wanapaswa kuombwa radhi kwani hakuna mwenye uwezo wa kuchezea barua pepe na hawakufanya hivyo, kwa asilimia mia moja.