Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiagana na Ujumbe kutoka Benki ya Stanbic, waliofika ofisini kwake mjini Dodoma, kueleza nia yao ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini. Kushoto kwa Waziri ni Mbunge wa Sumbawanga, Aeshi Hillary.
Na Veronica Simba - Dodoma
Wawekezaji mbalimbali wamemtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ofisini kwake mjini Dodoma na kumweleza nia yao ya kuwekeza kwenye miradi mbalimbali katika sekta ya nishati nchini.
Akizungumza na Waziri Muhongo, mwakilishi wa Kampuni ya L&T ya India, Sanjay Gupta aliwasilisha nia ya Kampuni hiyo ya kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Stanbic, Thomas Buonga akiwa ameambatana na Mkuu wa Sekta inayoshughulikia masuala ya Umma wa Benki hiyo, Noella Kimaro, walimweleza Waziri kuwa wanaangalia fursa ya kuwekeza katika miradi ya sekta ya nishati.
Naye, mwekezaji kutoka Denmark, Malte Meyer, akiwa amefuatana na Ofisa kutoka ubalozi wa nchi hiyo, Derrick Katunzi, alisema nia ya kampuni yake ni kuwekeza katika sekta ya nishati hususan uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo.
Waziri Muhongo aliwakaribisha wawekezaji hao na kuwahakikishia kupata ushirikiano kutoka serikalini endapo watakidhi vigezo stahiki vya uwekezaji vilivyowekwa. |
0 Comments