WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema wizara yake ipo mbioni kuwasilisha hoja ya kuandaliwa kwa muswada wa kuwa na sheria itakayosimamia uzalishaji wa kilimo cha mazao ya aina mbalimbnali wakiwemo ya chakula.

Lengo la sheria hiyo ni kuweka usimamizi mzuri utakaowalazimisha wakulima kufuata kanuni bora na taratibu wa uzalishaji zao husika na pia itawabana maofisa kilimo na ugani wa ngazi zote kuwajibika kwa wakulima maeneo ya uzalishaji ili kilimo kilete tija nchini.
Dk Tizeba alisema hayo katika Kampasi ya Solomon Mahlangu (Mazimbu) ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) wakati wa hotuba yake ya Mhadhara wa 14 wa kumbukizi ya miaka 33 tangu kifo cha Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine.
Licha ya kumtaja Sokoine kwamba alikuwa ni kiongozi mpenda maendeleo ya wananchi wa rika zote, Dk Tizeba alisema pia kiongozi huyo alihimiza kilimo na kutamani kuona tofauti ya kipato kati maskini na matajiri inapungua.
Alisema kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo, ni vyema sheria ikatungwa ambayo itasimamia uwajibikaji kwa pande zote wakulima na maofisa kilimo na ugani wa ngazi mbalimbali kutokana na kubanwa na sheria hiyo.
“Sheria ilikuwepo ya mazao, lakini zikandolewa na wakulima sasa wanalima bila kufuata kanuni za zao husika jambo linalichangia kushuka kwa uzalishaji wenye tija na hii kuwafanya maofisa kilimo na ugani kutowajibika upasavyo kwao,” alisema Dk Tizeba.