TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imefanikiwa kuokoa zaidi Sh bilioni 12.3 mwaka huu wa fedha, Sh milioni 912 kati ya hizo kutoka katika mishahara hewa.
Aidha, imepanga kuendelea na kesi 409 zilizopo mahakamani, zikiwa ni sehemu ya kesi 706 zilizoendeshwa, zikiwamo mpya 227.

Katika kipindi hicho, kesi 264 ziliamuliwa mahakamani ambapo kati ya hizo, kesi 161 watuhumiwa wake waliachiwa huru na kesi 103 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo au kulipa faini.
Aidha, kesi 33 ziliondolewa mahakamani kutokana na sababu mbalimbali.
Hayo yalisemwa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki alipokuwa anawasilisha makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka wa Fedha wa 2017/2018 aliyeomba kuidhinishiwa jumal ya Sh 821,322,347,674 (Sh bilioni 831.3).
Kati ya fedha hizo, Sh 390,970,890,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo wakati Sh 430, 351,457,674 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Alisema fedha nyingine zilizookolewa na kurejeshewa serikalini ni Sh bilioni 8.003 zilizotokana na ukwepaji ushuru kupitia mfumo wa kielektroniki wa EFDs, Sh bilioni 2.6 kutokana na ubadhirifu. Kiasi cha Sh milioni 794.18 ziliokolewa katika maeneo mengine.
Aidha, alisema kutokana na kuimarika kwa kitengo cha ufuatiliaji na urejeshaji wa mali, Takukuru imefanikiwa kutaifisha nyumba 6, ambapo 5 ziko Buhongwa na nyingine Ilemela, mkoani Mwanza.
Imetaifisha pia magari manne, mawili aina ya Toyota Chaser, jingine Toyota Land Cruiser na Mitsubishi Fuso yaliyopatikana kwa njia ya rushwa.
Kairuki aliongeza kuwa, Takukuru imefanya utafiti wenye lengo la kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mianya ya rushwa katika sekta za uhamiaji na afya.
Utafiti huo umehusisha uchambuzi wa mianya ya rushwa katika mfumo wa utoaji wa hati za kusafiria na tathimini ya uzingatiaji wa sheria na kanuni za uanzishaji na usimamizi wa maduka ya dawa muhimu.
Vyeti feki Waziri Kairuki alizungumzia utendaji wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, alisema imeendelea kufanya kazi yake kwa weledi na kwamba katika uhakiki wa vyeti vya waombaji wa kazi 39,511, vyeti vya waombaji 1,951 vilibainika kuwa ni vya kughushi na wahusika waliondolewa katika mchakato huku vyeti vikichukuliwa na kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Alisema Sekretarieti imekamilisha maandalizi ya kuunganisha mfumo wa maombi ya kazi na ule wa kutunza taarifa za wananchi unaomilikiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuhakiki kuwa wanaoajiriwa wanakuwa na sifa stahiki.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alisema malalamiko 186 ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa umma yalipokelewa na kuchambuliwa, kati ya hayto 130 yalihusu Sheria ya Maadili ya Viongozi na malalamiko, mengine 56 yakiwa hayahusiani na sheria hiyo.
Aliyataja baadhi ya malalamiko hayo kuwa ni pamoja na rushwa, jinai, migogoro ya ardhi na mengineyo. Malalamiko 9 yameshafanyiwa uchunguzi wakati wengine 121 yapo katika hatua mbalimbali za kiuchunguzi.
Kuhusu malalamiko 56 ambayo hayakuhusu ukiukwaji wa Shria ya Maadili ya viongozi wa Umma, walalamikaji walipewa ushauri na mengi yakielekezwa kwenye mamlaka husika.
Aliongeza kuwa, utafiti kuhusu hali ya maadili ya viongozi wa umma ulifanyika na matokeo kuonesha kuwa, yapo malalamiko ya matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa umma kwa asilimia 39 na matumizi mabaya ya mali za umma kwa asilimia 20.
Aidha, asilimia 70 ya waliohojiwa wana uelewa kuhusu masuala ya mgongano wa maslahi. Utafiti huo uliofanyika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mtwara, Arusha, Iringa, Mwanza, Shinyanga na Singida ulihusisha viongozi wa umma 573, wananchi 1,625, kampuni binafsi 62 na Asasi za Kiraia (Azaki) 50.