KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amelitaka Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kuzikatia huduma za maji taasisi ambazo ni wadaiwa sugu.
Profesa Mkumbo ametoa agiO hilo Dar es Salaam alipotembelea Dawasco na kuzungumza na wakuu wa idara wa shirika hilo pamoja na wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka(Dawasa).

“Haiwezekani wananchi wa kawaida wanaopata maji wanalipa tena wanatafuta hela kwa shida… iweje ziwepo taasisi ambazo hazilipi, Rais John Magufuli alishatoa maelekezo ya kukata umeme kwa wasiolipa na hiyo haikuhusu Tanesco tu, bali taasisi zote zinazotoa huduma,” amesema.
Amesema sasa ni lazima kuwepo na usimamizi madhubuti ili taasisi zinazodaiwa ankara za maji zilipe kwa wakati ili fedha hizo zitumike kuboresha zaidi huduma katika Jjiji la Dar es Salaam.
“Taasisi zote ambazo hazijalipa zikatiwe kama alivyoelekeza Rais, wanatakiwa walipe ili tuendelee kuwekeza katika miundombinu hii. Hakikisheni taasisi zote zinalipa ankara zao ili muwe na uwezo wa kufanya kazi na kuwekeza katika miundombinu,” amesema.
Aidha alisema bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama katika jiji la Dar es Salaam ingawa kazi kubwa imefanyika kuhakikisha wananchi wengi wa hilo wanapata maji huku hitaji likiwa ni lita milioni 510 kwa siku.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, hatua zinazochukuliwa sasa zitawezesha upatikanaji wa maji kufikia lita milioni 520 kazi ambayo ni kubwa.
“Kazi tunayokwenda kusukuma na kuongeza nguvu ni kuhakikisha kwamba tunasambaza maji kwa wingi na kwa kasi zaidi, hivyo natoa mwito tuwekeze zaidi kwenye suala la usambazaji na Serikali tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya miundombinu,” amesema.
Alitoa mwito wa kuwapo usimamizi mzuri wa miradi ili ikamilike na kuanza kutumika kwa wakati uliopangwa.
“Kwa miaka 50 ya Uhuru jiji kama la Dar es Salaam lina tatizo kubwa la maji hiyo ni aibu, hatupaswi kutembea, bali tunatakiwa kukimbia ili watu wapate maji.”
“Ingawa malengo yetu ni kwamba ifikapo 2020 tuweze kufikia asilimia 95 ya watu kupata maji, sisi tunapaswa kuhakikisha wananchi wetu wote wanapata maji safi na salama,” alisema.
Aidha alisema maji yanapotea kwa kiasi kikubwa hivyo inabidi kuwekeza elimu kwa umma na kuwafahamisha kwamba maji ni bidhaa adimu ili wayatunze na penye tatizo wachukue hatua stahiki mapema.
“Pamoja na kwamba malengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo 2020, tujitahidi tufikie asilimia 100 ya usambazaji wa maji kabla ya 2020, ili baadae tuwekeze nguvu nyingi vijijini na hili linawezekana. Tuhakikishe tunasimamia miradi ya maji ili matokeo yake yaonekane,” alisema.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco, Cyprian Luhemeja alisema pamoja na uzalishaji mkubwa wa maji, ipo changamoto ya usambazaji.
Alisema Shirika hilo lipo katika mkakati wa siku 90 kuhakikisha linaboresha upatikanaji wa huduma za maji safi na salama jijini.