Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Apr 28, 2017

TEF yataka Profesa Lipumba kutoa tamko

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba kutoa tamko kuhusu shambulio lililofanywa Jumamosi iliyopita jijini Dar es Salaam na walinzi wa chama hicho wanaomuunga mkono, dhidi ya wanahabari.

Aidha, TEF imewaagiza wanahabari nchini kuchukua tahadhari wakati wote wanapofanya kazi kwenye mikutano ya wanasiasa au vyama vya siasa vinavyopenda kuita idadi kubwa ya wafuasi, ili kuhudhuria mikutano hiyo, kwa sababu mara nyingi usalama katika mikutano hiyo huwa mdogo. Akitoa tamko hilo Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema Jukwaa la Wahariri linalaani shambulio hilo dhidi ya wanahabari, kuwapa pole walioshambuliwa na kumtaka Profesa Lipumba atoe tamko kuhusu tukio hilo mapema iwezekanavyo.
Taarifa zinaonesha kuwa wanahabari walioshambuliwa katika ukumbi wa mikutano, ndani ya hoteli ya Vina iliyopo Mtaa wa Makutano –Kigogo Mburahati jijini humo, saa 5 asubuhi, walikuwa wakitekeleza jukumu lao la kisheria la kukusanya habari, kwa ajili ya kuutaarifu umma kuhusu kilichojiri kwenye mkutano huo unaodaiwa kuitishwa na viongozi wasiomuunga mkono Profesa Lipumba na kuhudhuriwa na wafuasi wa Cuf wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mashuhuda wa tukio hilo wakiwemo wana Cuf waliokuwa mkutanoni na kushambuliwa, walisema kwa nyakati tofauti kuwa uvamizi na shambulio hilo lilitekelezwa ili kuhakikisha mkutano wa wasio wafuasi wa Profesa Lipumba unavurugika, hatua iliyotekelezwa na walinzi wa Cuf ya Lipumba bila kutofautisha wanahabari na wanachama na matokeo yake kuumiza kila aliyekuwemo.
Wakati akizungumza na gazeti hili kwenye Makao Makuu ya Cuf, Buguruni Dar es Salaam saa chache baada ya shambulio hilo, Mkurugenzi wa Habari wa CUF Taifa, Abdul Kambaya alikiri kuwa walinzi waliokwenda katika hoteli hiyo siku ya shambulio ni wa chama hicho. Alisema walikuwa wakitekeleza jukumu lao la kukilinda chama, kuitetea katiba ya chama hicho na kulinda viongozi wao akiwemo Profesa Lipumba dhidi ya watu wanaokula njama kumpindua au kutekeleza jambo lolote kinyume na uongozi wake, wakiwemo waliokuwa wakifanya mkutano huo wa Vina hoteli aliosema kuwa ni batili.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa TEF, wakati wowote baada ya kumsikia Profesa Lipumba, watatoa uamuzi kuhusu suala hilo. Alisema haitachukua wiki mbili kabla ya kueleza uamuzi huo. “Kwa sababu wanahabari wameshambuliwa na Profesa Lipumba hajatekeleza ahadi yake ya kutoa tamko lake juzi, leo (jana) sisi tumetoa letu na tunampa muda wakati tukiandaa uamuzi wetu ili aseme jambo,” alisema Makunga.
Aliweka bayana kuwa Maalim Seif alikwishaandika barua kulaani shambulio hilo na kuwapa pole wanahabari waliopigwa na kuumizwa, miongoni mwao akiwemo Fred Mwanjala (Channel Ten), Asha Bani (Mtanzania), Mary Geoffrey (Nipashe), Mariam Mziwanda (Uhuru), Kalunde Jamal (Mwananchi), Rachel Chizoza (Clouds Media) na Henry Mwang’onde wa The Guardian. Kutokana na maelezo ya Makunga, Jukwaa hilo limeiweka Cuf katika uangalizi, huku likiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mikutano ya Profesa Lipumba, wafuasi wake na wanahabari wanaowaalika.
Alikitaka chama hicho na Watanzania kwa ujumla kufahamu kuwa kuzuia au kupiga wanahabari wakiwa kazini ni kosa la kisheria linaloweza kumsababisha mhusika ashitakiwe kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya 2016. Katibu wa TEF, Neville Meena aliwakumbusha wanahabari nchini kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari wakati wote wanapokuwa kazini, hasa katika mikutano ya vyama vya siasa vyenye tabia ya kuandaa mikutano na wanahabari na kualika wafuasi wengi wa vyama hivyo kuwa sehemu ya waalikwa wa mkutano.
Meena alisema uzoefu unaonesha kuwa penye mikutano ya wanahabari na viongozi wa vyama vya siasa, ambako wafuasi wa vyama hivyo wanakuwa sehemu ya wahudhuriaji, usalama unakuwa mdogo hivyo, wanahabari wachukue tahadhari kuhusu usalama wao, vifaa vyao vya kazi na kuwa na mshikamano pindi lolote baya linapofanywa dhidi yao.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP