Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.
NAIBU Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema hakuna sababu ya Bunge kuahirisha shughuli zake za kawaida ili kujadili vitendo vya kutekwa kwa watu kama ilivyoombwa na wabunge; kwa vile suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya sheria.

Dk Tulia alitoa msimamo huo wakati akijibu mwongozo wa wabunge watatu waliosimama mara baada ya kipindi cha maswali na majibu wakihoji msimamo wa kiti cha Spika katika mwendelezo wa vitendo vya kutekwa kwa watu mbalimbali, mmoja akidai wabunge 11 wamo katika mpango wa kutekwa.
Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM) na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) walitumia Kanuni ya 47 kuomba mwongozo kwa suala hilo huku Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema) akitumia Kanuni ya 68 (7).
Katika ombi lake la mwongozo, Bashe aliomba Bunge kuahirisha shughuli zake za jana ili kujadili vitendo vya utekaji wa watu huku akisema anazo taarifa kutoka kwa mawaziri (bila kuwataja) kuwa kuna orodha ya wabunge 11 walio katika mpango wa kutekwa.
“Mheshimiwa Naibu Spika natumia Kanuni ya 47 kanuni ndogo ya (1), (2) na (3) na wewe unaweza kutumia kanuni ndogo ya (4) ili kuruhusu shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili suala la kutekwa ovyo kwa watu.
“Kipo kikundi cha watu ambacho hakijafahamika, kimekuwa kikiteka watu. Kikundi hiki kilimteka Msukuma (Joseph Kasheku Msukuma – Mbunge wa Geita Vijijini), kilimteka Bashe na pia Malima (Adam) wakati wa mikutano ya CCM.
“Kikundi hiki nadhani ndicho pia kilichomteka Ben Saanane (Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe), na juzi kilimteka msanii Roma Mkatoli (Ibrahim Mussa – msanii maarufu wa Hip Hop).
Naomba suala hili lichukuliwe kama jambo la dharura na Bunge liahirishe shughuli zake ili tujadili suala hili ambalo limeanza kuwatia hofu Watanzania,” alisema Bashe na kuongeza: “Nasema hivyo kwa sababu hatujui ni Watanzania wangapi wa ngazi za chini wametekwa na kikundi hiki hadi sasa.
Wapo baadhi ya mawaziri wameniambia kuna orodha ya wabunge kumi na moja walio katika orodha ya kutekwa nikiwemo mimi na wameniambia niwe makini niwapo barabarani.
“Chama changu cha CCM kiliomba ridhaa kwa Watanzania ili kuwaongoza na si kuwahatarishia maisha. Naomba Bunge liunde Tume au tutumie Kamati yetu ya Bunge ya Usalama ili kuchunguza suala hili. Hali si salama, hakuna hope (matumaini).”
Naye Mbilinyi akiomba mwongozo kwa suala hilo alisema; “Taifa lipo gizani, kumezuka utamaduni mpya, utamaduni wa kimafia, ni utaratibu uliokuwepo miaka ya zamani sana wakati ule alitekwa Kassim Hanga Zanzibar, lakini ukatoweka, na sasa umerudi.
“Tangu utamaduni huu uanze Jeshi la Polisi wamekuwa wanasema hawajui waliko watu waliotekwa. Lipo tukio la kutowekwa Ben Saanane, tukio la kukutwa kwa maiti za watu sita au saba kwenye viroba katika Mto Ruvu na wakazikwa bila kufanyiwa uchunguzi.
“Nape (Nnauye – Mbunge wa Mtama) naye alitekwa na mtu mwenye bastola bahati nzuri akaokolewa na Maulid Kitenge (mtangazaji wa E FM).
“Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu Nchemba) kama mambo yanafanyika na hupewi taarifa au unashinikizwa, ni vizuri ukajiuzulu.
Wewe ni mtu wa kiwango cha juu maana uligombea urais na bado una future mbele yako, unaweza kujiuzulu na siku za usoni ukawa Rais.
“Rais Mwinyi (Ali Hassan – Rais mstaafu) aliwahi kujiuzulu miaka ya 1976 kwa makosa yaliyofanywa na watendaji wa chini yake lakini akarudi kama shujaa miaka ya 1980 na kuwa Rais wa nchi hii. Na wewe kwanini usifanye hivyo ili kulinda heshima yako?” alihoji Mbilinyi.
Naye Minja akitumia Kanuni namba 68 (7) aliomba mwongozo wa Naibu Spika akisema saa 5 asubuhi juzi, askari wenye silaha za moto walivamia na kuzingira nyumba yake iliyopo mjini Morogoro wakiwa na lengo la kumkamata mbunge huyo.
Alisema polisi hao walifanya hivyo pasipo kumpa taarifa yeye ambaye ni kiongozi na kuwa hatua hiyo imeleta tafrani na sintofahamu kwa familia yake pamoja na kuwa hawakumkamata kutokana na kuwa bungeni mjini hapa.
Akijibu mwongozi wa Bashe na Mbilinyi, Naibu Spika Dk Tulia alisema isingewezekana kwa Bunge kuahirisha shughuli zake ili kujadili suala hilo kwa vile vyombo vya sheria vinashughulikia suala hilo.
Alisema kimsingi ili kuielewa kanuni ya 47 iliyotumiwa na wabunge katika kuomba mwongozo huo, ni lazima kanuni hiyo isomwe na kanuni ya 48 kifungu kidogo cha 4 kinachofafanua ni jambo lipi linaweza kuhesabiwa na Bunge kuwa ni la dharura.
Alisema kanuni hiyo inafafanua vizuri kwamba jambo litahesabika kuwa ni la dharura endapo litakuwa na maslahi kwa taifa na litakuwa halijashughulikiwa na vyombo vya kisheria na kwamba jambo la utekaji nyara kwa wananchi si la dharura kwa vile linashughulikiwa na vyombo ya sheria na utaratibu wa kawaida wa kisheria utatumika katika kulishughulikia.
Kuhusu mwongozo wa kuvamiwa kwa makazi ya Mbunge Minja, Naibu Spika alisema asingeweza kulitolea mwongozo kwa vile kwa mujibu wa Kanuni ya 67 (8) Spika anapaswa kutolea mwongozo kwa suala ambalo limetokea mapema bungeni.