Vikosi vinane vitakavyoshiriki michuano ya 12 Fainali za Kombe la mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 nchini Gabon 2017 vimetajwa.Michuano hiyo inatarajiwa kuanza Mei 14 hadi 28 mwaka huu katika miji ya Libreville na Franceville nchini humo na kila timu itakuwa na wachezaji 21 kikosini.
Timu nane zimegawanywa katika makundi mawili, A likiundwa na wenyeji Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana na B likiundwa na Mali, Tanzania, Angola na Niger.
Timu mbili za juu katika kila kundi zitafuzu moja kwa moja Fainali za Kombe la Dunia, ambazo zitafanyika nchini India kuanzia Oktoba 6 hadi 28, mwaka huu.
Awali, michuano hiyo ilikuwa ifanyike nchini Madagascar kuanzia Aprili 2 hadi 16, mwaka huu, lakini Kamati ya Utendahji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) chini ya Rais wa zamani, Mcameroon Issa Hayatou ikaipokonya uenyeji nchi hiyo Januari 12 baada ya taarifa za wakaguzi.
Na Februari 3, mwaka huu, Gabon wakapewa uenyeji wa fainali hizo. Hivyo Gabon wakachukua nafasi ya Madagascar na Tanzania ikachukua nafasi ya Kongo iliyoenguliwa kwa kutumia mchezaji aliyezidi umri.
Mali nayo iliondolewa baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuifungia nchi hiyo kufuatia Serikali yake kuwafukzua madarakani viongozi wa chama cha soka na Ethiopia wakapewa nafasi, kabla ya kurejeshwa kufuatia kuwarudisha viongozi hao.
|
0 Comments