Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo
FAMILIA ya Jonathan Kalambwia (55) wa Kata ya Sokoni II, Kijiji cha Ng’iresi wilayani Arumeru imepoteza watoto wake wote watano wakiwemo wanafunzi wawili kutokana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya mkoa huo.

Tukio hili limetokea wakati simanzi na majonzi ya vifo vya wanafunzi 33 na watumishi watatu wa Shule ya Lucky Vincent ya Arusha zikiendelea, majonzi yameukumba tena Mkoa wa Arusha baada ya Saa saba usiku wa kuamkia jana, katika eneo hilo la Ng’iresi mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mfululizo mkoani hapa, zilisababisha maafa kwa familia ya Kalambwia baada ya mti uliokuwa katika mlima Lake Mana kung’oka na kuangukia nyumba ya mzee huyo iliyokuwa chini ya mlima huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo (pichani) alisema kati ya watoto hao watano, wawili ni wanafunzi. Baba yao ni mlinzi wa Hospitali ya Dk Mohamed ya jijini Arusha. Kamanda Mkumbo aliwatajaja wanafunzi ambao ni watoto wa Kalambwia ambaye siku ya tukio alikuwa kazini ni Miriam Jonathan (16) wa Kidato cha Pili wa Shule ya Sekondari ya Inaboishu na Gloria Jonathani (11) ambaye ni wa Shule ya Msingi Ng’iresi iliyoko wilayani Arumeru.
Alisema watoto wengine waliokufa ni mtoto wa kwanza, Giliad Jonathan (31), Lazaro Jonathan (26) na Best Jonathan (20). Mama wa watoto hao hakuwapo wakati wa ajali hiyo. Kamanda Mkumbo alisema mti huo uliokuwa katika mlima wa Lake Mana uliangukia nyumba hiyo baada ya kung’olewa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika Jiji la Arusha na mkoa kwa ujumla.
Aliipa pole familia ya mzee huyo kwani tukio hilo ni majonzi makubwa kwake kwani familia nzima imeondoka na kumtaka kuwa na uvumilivu. Kamanda Mkumbo alitoa mwito na ushauri kwa wakazi wa Arusha kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kwa kukarabati nyumba zao na kuacha kujenga chini ya mti ama kwenye vyanzo vya maji.
Alisema kujenga katika vyanzo vya maji ama chini ya mti ni kujitafutia majanga mengine hivyo ni vema kila mkazi wa Mkoa wa Arusha kuchukua tahadhali hiyo.