MAMLAKA ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) iliyovunjwa na Rais John Magufuli hivi karibuni imekabidhi mali rasmi zake kwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ikiwemo watumishi 284, nyumba, magari na kubadilisha majina ya majengo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira katika Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma, Anselm Kutika alisema jana miongoni mwa yaliyofanyika ni kubadilisha CDA kuwa Manispaa ya Dodoma wakianzia na ofisi za makao makuu yake.
Kutika alisema Mei 19, walikabidhiwa mali zote za CDA katika makabidhiano ya awali yaliyohusisha jengo la makao makuu ya CDA lililowekwa nembo ya Manispaa Dodoma. Alisema magari yaliyokuwa yakitumiwa na CDA, malori, magreda, mazima na mabovu zaidi ya 28 sasa yamehifadhiwa kwenye yadi ya manispaa ya Dodoma.
“Tumekabidhiwa majengo yakiwemo maghorofa yaliyopo eneo la Kikuyu, tumekabidhiwa nyumba za Msajili wa Majumba zaidi ya 450,” alieleza. Mwenyekiti huyo alisema Kikuyu pekee wamekabidhiwa nyumba 144 zilizofanyiwa matengenezo na 148 zilizo kwenye matengenezo na zitakamilika Juni 30, 2017.
Pia alisema wamekabidhiwa karakana ya kufyatulia matofali iliyopo Kizota, nyenzo za ujenzi kama tingatinga, malori ya mchanga na matangi ya maji. Kutika ambaye ni Diwani wa Kikuyu Kusini alisema sasa kutakuwa na Mkurugenzi wa Manispaa.
“Kila mfanyakazi atabaki kwenye nafasi yake, jengo la CDA sasa litakuwa la manispaa na kila mtu atabaki kwenye kitengo chake,” alisema. Alisema usimamizi wa Manispaa utaboreshwa na mtendaji atakuwa ni mkurugenzi akisimamiwa na madiwani.
Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jumanne Ngede alisema walishuhudia kusainiwa kwa mkataba wa makabidhiano kati ya CDA na manispaa hiyo. Alisema kinachofanyika ni utekelezaji wa agizo la Rais na hakuna mtumishi atakayeguswa kwenye ajira na wote ajira zao zitatambulika kwa kada za manispaa.
“Tutawachukua watumishi tutakaowahitaji na wengine watakabidhiwa kwa wizara nyingine watakazokuwa wamepangiwa,” alisema Ngede na kuongeza kuwa kazi zote zitakwenda sawa sawa na mji utapangika vizuri na kazi ya uendelezaji, ustawishaji, usimamizi na udhibiti utafanyika ili mji uendelee kuwa mzuri na uliopangika vyema.