WAFANYABIASHARA na abiria wanaotumia kituo cha magari ya kwenda Bahi, Manyoni na Itigi kilichopo Mnadani kata ya Kizota, Manispaa ya Dodoma wamelalamikia harufu kali inayotoka kwenye kiwanda cha kusindika nyama ya punda kilicho karibu na eneo hilo.

Wamesema harufu mbaya na inzi wengi kituoni hapo imekuwa ikiwakimbiza wateja na hivyo kujikuta wakifanya biashara kwa hasara. Pia wamelalamikia tozo la choo na ukosefu wa maeneo ya kupumzikia abiria. Wakizungumza kituoni hapo juzi mmoja wa wafanyabiashara hao Khadija Rweyongeza anayeuza chakula, alisema hali ya harufu mbaya inayotokea kiwanda cha kusindika nyama ya punda inasababisha kukosa wateja wa kula chakula katika maeneo hayo.
“Hali ya biashara ni mbaya kituo hiki kinatumiwa na abiria wa kwenda Bahi, Manyoni na Itigi lakini abiria wakishuka kwenye daladala kutoka mjini hawatamani hata kula chakula kutokana na eneo hili kuwa na harufu mbaya,” alisema. Alisema suala hilo mara kadhaa wamelifikisha kwenye uongozi, lakini hawaoni tatizo hilo likitatuliwa. Nao waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda katika eneo hilo wamesema hali ya biashara kwao ni mbaya kutokana na sasa kituo hicho kupata abiria wachache. Dereva Awadhi Salum alisema abiria wengine wanaamua kupanda magari makubwa ya kwenda Singida ili washuke Manyoni ili wasifike kituoni hapo.
“Tatizo hili liangaliwe kwa makini kwani stendi hii ilihamishiwa hapo kutokea Mjini lakini wahusika wafuatile mazingira ya wafanyabiashara wa hapa,” alisema Naye dereva mwingine Juma Hassan, alisema tozo ya Sh 200 ya huduma ya choo ni kubwa kulinganisha na kipato chao cha kila siku hivyo kupelekea uchafuzi wa mazingira kwa watu kujisaidia kwenye vichaka. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa eneo hilo, Amos Msote amethibitisha kuwepo kwa matatizo hayo na kuwa wameshawasilisha sehemu husika na kuwa wanasubiri utekelezaji wa changamoto hizo.
Aidha diwani wa Kizota, Jamali Yaled, akijibu changamoto hizo alisisitiza kuwa tozo ya Sh 200 ni sahihi na itaiendelea kutozwa na endapo mtu atakaidi na kujisaidia ovyo atatozwa faini ya Sh 50,000 kwa kosa moja. Kuhusu tatizo la harufu mbaya inayotoka katika kiwanda cha kusindika nyama ya punda katika maeneo hayo taarifa zimeshafikishwa katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC). “Wao ndio watatoa maamuzi,” alisema.