KUTOKANA na kufukuzwa kazi kwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambrose Mtarazaki amewataka watumishi wengine waliopo katika wilaya hiyo waondokane na tabia ya wizi wa mali za umma na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

“Taswira mpya ni kufanya kazi kwa misingi ya utawala bora inayotaka Serikali hii ya Awamu ya Tano na sio muda mwingi kufikiria vitendo viovu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi wetu,” alisema Mtazaraki. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha kikao cha Baraza la Madiwani mwishoni mwa wiki, mwenyekiti huyo alitoa rai kwa watumishi hao kwamba hivi sasa wanapaswa kubadilika na sio kila siku wanakuwa ni watu ambao wanafanya makosa kwa makusudi huku wakijiua kwamba wanaumiza wananchi.
Alisisitiza kuwa yeye na madiwani wenzake wamefikia hatua ya kuwafukuza kazi watumishi wanne waliobainika kufanya makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umma ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo. Vilevile aliwataka pia madiwani wahakikishe wanajitambua katika nafasi zao walizonazo kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kwenye maeneo yao ili ijengwe kwa viwango vinavyokubalika.
Pamoja na mambo mengine, watumishi waliofukuzwa kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kuwa ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kitura, Daniel Komba aliyefukuzwa kazi kutokana na kufanya matendo kinyume cha dhamira njema kwa kughushi risiti za marejesho ya fedha Sh 350,000 za michango ya wananchi wa kata hiyo. Ilibainishwa kuwa fedha hizo walikuwa wamechanga wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao na kwamba risiti aliyoitumia kukusanyia fedha hizo haikuwa risiti halali ya serikali.