Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mzee Benjamin Mkapa amevikosoa vyombo vya habari barani Afrika na haswa kusini mwa Jangwa la Sahari kwa kile alichosema vingi vimejikita katika kuripoti habari za kisiasa na matukio ya nani kafanya nini au kawa nani, badala ya kuripoti habari za uchumi za kuwasaidia wananchi.
Mzee Mkapa aliyasema hayo alipokuwa akifanya mahijiano na na Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) ya nchini Ujerumani ambapo alisema kwenye vyombo vya habari vya Afrika kuna upungufu mkubwa wa wa habari za uchumi na maendeleo zilizofanyiwa utafiti wa kina.
“Tatizo moja kubwa la vyombo vya habari vya nchi za Afrika hasa hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ni kwamba habari nyingi zinazopewa kipaumbele ni zile za kisiasa na zinazohusu nani ni nani na kafanya nini.”
 
“Kuna upungufu mkubwa wa habari za kiuchumi na maendeleo zilizofanyiwa utafiti wa kina na zinazochochea maendeleo. Kuna habari kidogo sana za utetezi wa kimaendeleo na kujipanga ili tupige hatua.”
Kufuatia hali hiyo, Mzee Mkapa alisema kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaodaiwa kuwa umebanwa, unahusu vyombo vya habari ambavyo havina mchango kwenye maendeleo ya uchumi wetu zaidi ya kuzungumzia matokeo badala ya uchambuzi.
“Kwa hiyo, huo uhuru wa vyombo vya habari unaosema unabanwa unahusu kundi la vyombo vya habari ambavyo havina mchango wowote katika uchambuzi wa masuala ya uchumi utetezi wa maendeleo wala kwenye kujipanga kujitafutia maendeleo. Nasi ni taifa masikini linalohitaji kuendelea. Nadhani ni uamuzi sahihi.”  alisema Mzee Mkapa.
Kauli hii ya Mzee Mkapa ilikuja baada ya kuulizwa kuhusu madai ya kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inabana uhuru wa vyombo vya habari hali ambayo haikuwapo miaka ya nyuma.