Maajenti wa Marekani na Korea Kusini wanapanga njama ya kumuua kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, vyombo vya habari nchini humo vimesema.
Taarifa kutoka wizara ya usalama nchini Korea Kusini imesema mawakala wa kundi la kigaidi linaloungwa mkono na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na shirika la ujasusi la Korea Kusini wameingia nchini Korea Kusini wakiwa na silaha hatari ya bio-kemikali.
Taarifa hiyo imesema Korea Kaskazini itawasaka mawakala hao na kuwaangamiza bila huruma.
Korea Kaskazini imesema hayo huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka katika rasi ya Korea.
Taarifa hiyo, ambayo imechapishwa na shirika la habari la Korea Kaskazini inasema njama hiyo inahusisha kutumiwa kwa "silaha ya bio-kemikali pamoja na kemikali yenye miali nururishi na sumu".
Matokeo ya shambulio kama hilo yataanza kubainika baada ya miezi sita hadi 12, taarifa hiyo imesema.
Vita vya maneno kati ya Marekani na Korea Kaskazini vimezidi wiki za karibuni.
Korea Kaskazini imetishia kufanya jaribio la sita la silaha za nyuklia.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka siku za karibuni, huku Korea Kaskazini na Kusini zikifanya mazoezi ya kijeshi.
Mwishoni mwa wiki, Rais Marekani Donald Trump alisema angependa kukutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un, iwapo kungekuwa na mazingira mahsusi.
Amesema ingekuwa "heshima kuu kwake".
"Kungelikuwa na hali mahsusi kwangu kukutana naye, ningekutana naye - bila shaka. Ingekuwa heshima kuu kwangu kufanya hivyo," Bw Trump aliambia shirika la habari la Bloomberg Jumatano.
Jumapili, alikuwa amemwelezea Bw Kim kama "kijana mwerevu".
Lakini Ikulu ya White House baadaye ilitoa taarifa kufafanua matamshi ya Bw Trump na kusema Korea Kaskazini ingehitaji kutimisha masharti mengi kabla ya mkutano kati ya viongozi hao wawili kufanyika.
Marekani imetuma meli za kivita na nyambizi eneo hilo na pia imeweka mtambo wa kutungua makombora ya adui Korea Kusini, mtambo ambao maafisa wanasema umeanza kufanya kazi.
Jumapili, makala katika shirika la habari la serikali ya Korea Kusini KCNA ilitoa wito kwa Marekani kutafakari kuhusu "madhara makubwa ambayo yanaweza kusababisha na uchokozi wake wa kipumbavu wa kijeshi."
Korea Kaskazini imekuwa ikifanya majaribio ya makombora mara kwa mara miezi ya karibu na imekuwa ikitishia kufanya jaribio la silaha za nyuklia kwa mara ya sita.Rais Trump aliambia CBS kuwa Marekani "haitakuwa na furaha sana" iwapo majaribio zaidi yatatekelezwa na Korea Kaskazini.
Alipoulizwa iwapo hili litasababisha hatua ya kijeshi kutoka kwa Marekani, alijibu: "Sijui mimi. Naam, tusubiri tuone."
Pyongyang kwa muda mrefu imeamini kwamba inahitaji silaha za nyuklia ili kujilinda, na imekuwa tayari kukabiliana na vitisho na adhabu kutoka kwa jamii ya kimataifa.
Kim Jong Un ameonyesha kujitolea kwake, kinyume na babake na babu yake, kupuuza msimamo na maoni na mshirika pekee mkuu wa Korea Kaskazini, China.
Kiongozi wa mashauriano wa zamani wa Marekani Chris Hill anasema Kim Jong il (babake Kim Jong-un) alijali sana yale ambayo wengine walifikiria, na hasa Wachina. Lakini mwanawe Kim Jung Un hajali wasemayo watu.
0 Comments