WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hajaridhishwa na kasi ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi, unaofanywa na Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Lukuvi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza na madiwani na watumishi wa manispaa hiyo wakati wa ziara yake ya siku mbili jijini hapa.
Alisema hayo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, John Mwanga kutoa taarifa kwake ya ukusanyaji wa kodi ya ardhi iliyoonesha kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17, manispaa ilikusanya kiasi cha Sh bilioni 1.3 kati ya lengo la kukusanya kiasi cha Sh bilioni 2.5.
Alisema amesikitishwa kuona manispaa imetoa hati 800 tu kati ya hati 16,141 ambazo zingestahili kutolewa, ambazo ni viwanja halali ambavyo wamepimiwa wananchi na kustahili kupatiwa hati hizo kwa mujibu wa sheria ili serikali iweze kukusanya kodi ya ardhi. “Hapa hamjafanya vizuri, kodi ya ardhi ndiyo inayotupatia mapato ya kujenga miundombinu na miradi mingine ya maendeleo,” alisema Lukuvi.
Aliwataka Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Murunga na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, John Wanga kuhakikisha kuwa wananchi wote waliopimiwa viwanja wanapatiwa hati ili kuiwezesha serikali kukusanya kodi ya ardhi. “Mna wafanyakazi wa ardhi zaidi ya 40, lakini hati mlizotoa ni chini ya asilimia moja, mmekusanya bilioni 1.3 kama mapato hamjaitendea haki serikali, mlitakiwa muwe na walipa kodi wa ardhi 16,000 ambao hamjawapatia hati,” alisema Lukuvi na kuongeza: “Msipowapatia watu hawa 16,000 hati za kumiliki ardhi ili serikali iweze kukusanya kodi mtakuwa hamna maana kwa serikali na hadi Juni 30 mwaka huu wawe wamekabidhiwa hati za kumiliki ardhi”.
Meya wa Manispaa ya Ilemela, John Murunga alimhakikishia Lukuvi kuwa manispaa yake itahakikisha kuwa watu hao 16,141 waliopimiwa viwanja, wanapatiwa hati ili walipe kodi ya serikali. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alimpongeza waziri huyo kwa kazi nzuri, ambayo amekuwa akiifanya katika sekta ya ardhi. Alisema waziri huyo amedhamiria kuifanya sekta ya ardhi kuwa mkombozi wa shughuli za kiuchumi nchini. “Tangu uteuliwe kuwa waziri, sekta ya ardhi imepata mabadiliko makubwa,” alieleza.